NA JUMBE ISMAILLY ITIGI                 

MAMLKA ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) inatarajia kuongeza idadi ya askari wa mwitikio wa haraka (RRT) watakaoshirikiana na askari wengine wa kawaida kukabiliana na vitendo vya ujangili kwenye mapori ya akiba yaliyopo katika sehemu mbali mbali nchini.

Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori (TAWA) John Kaaya, aliyasema hayo kwenye taarifa aliyotoa kwenye hafla ya ufungaji wa mafunzo ya miezi miwili kwa walimu watano wa vikosi vya mwitikio wa haraka yaliyofadhiliwa na Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori (WCS) na kufanyika katika Kijiji cha Rungwa, tarafa ya Itigi, wilayani Manyoni.

Aidha Mhifadhi mkuu huyo alibainisha pia kuwa hali ya vitendo vya ujangili hapa nchini imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mbinu mbali mbali kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori (TAWA) pamoja na Mamlaka ya hifadhi za Ngorongoro katika kukabiliana na vitendo vya ujangili.  

“Kwa kweli hali ya ujangili nchini imepungua sana kutokana na mbinu mbali mbali ambazo mamlaka mbali mbali kama vile Tawa,Tanapa na Ngorongoro kushirikiana katika kukabiliana na vitendo vya ujangili”alisisitiza Kaaya ambaye ni mhifadhi mkuu waTawa.

Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori (WCS),Michael Lesdcha alikiri kuridhishwa na hali ya mambo  yanavyotekelezwa Tanzania kupitia ufadhili wanaotoa, na kutoa mfano wa mambo hayo kuwa ni kuanzishwa kwa vikosi vya askari wa mwitikio wa haraka na kuanzishwa kwa mikakati ya haraka ya kupambana na vitendo vya ujangili.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo msaidizi wa shirika la WCS lenye makao yake makuu katika bustani ya wanyamapori ya Bronx, Mji wa New York, Nchini Marekani, kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2013, kulikuwa na shida sana ya wanyamapori, hususani tembo.

Alisema mwaka huu wa 2021 takwimu zinaonyesha kwamba pori la Rungwa Kizigo Muhesi ni pori lenye wanyama wengi kuliko sehemu zote za Afrika ya Mashariki.