NA MARYAM HASSAN
SEIF Khamis Masoud (18) mkaazi wa Masingini Unguja, anatuhumiwa kwa makosa matatu ikiwemo kubaka, kutorosha na kumuingilia kinyume na maumbile mtoto wa kike mwenye umri wa miaka (16).
Mshitakiwa huyo, alifikishwa katika mahakama ya mkoa Mwera inayoshughulikia kesi za udhalilishaji mbele ya Hakimu, Taki Abdalla Habibu, na kusomewa kosa lake na Mwendesha Mashitaka wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka (DPP) Muzne Mbwana Suleiman.
Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba mshitakiwa mnamo mwezi Aprili tarehe isiyofahamika mwaka jana majira ya saa 3:00 za asubuhi huko Hanyegwa mchana Wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.
Mshitakiwa alimtorosha mtoto wa kike aliyechini ya uangalizi wa wazazi wake kutoka nyumbani kwao na kumpeleka katika nyumba ya kaka yake Hanywegwa mchana jambo ambalo ni kosa kisheria.
Aidha, Wakili huyo alidai kuwa mshitakiwa baada ya kumtorosha msichana huyo alimuingilia kimwili jambo ambalo ni kosa kisheria.
Pia mshitakiwa huyo anadaiwa kumuingilia kinyume na maumbile mtoto huyo, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Mshitakiwa baada ya kusomewa kosa lake alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana jambo ambalo lilikataliwa na upande wa mashitaka.
DPP huyo, alisema makosa aliyoshitakiwa nayo mshitakiwa hayana dhamana na badala yake aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupanga tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi kwa kuwa upelelezi umekamilika.
Hakimu Taki, alikubaliana na maelezo yaliyotolewa na upande wa mashitaka na kuamua kuahirisha shauri hilo hadi Juni 9, mwaka huu, kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi na mshitakiwa amepelekwa rumande.