NA TIMA SALEHE,DAR ES SALAAM
KIKOSI Cha Azam FC , kimeibuka kidedea kwa mabao 3-2 dhidi ya Kagera Sugar, katika mchezo wa ligi kuu ya vijana chini ya miaka 20, Tanzania Bara.
Mchezo huo ulipigwa juzi, kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Saa 3:00 usiku, baada ya kumalizika kwa mchezo wa Tanzania Prisons dhidi ya Mtibwa Sugar, ambapo Mtibwa ilipata ushindi wa bao 1-0.
Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha Mkuu wa timu hiyo, Bahati Vivier, alisema wamefurahi kupata ushindi huo, mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa.
Alisema anahitaji kufanya marekebisho zaidi katika eneo la umaliziaji, ambapo kumeonekana kuwa na shida kidogo kwa wachezaji wake, kutengeneza nafasi nyingi lakini umaliziaji tatizo.
Azam wapo kundi (B) wanashika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi nne, huku wapinzani wao Kagera wakiwa nafasi ya mwisho wakishindwa kuvuna pointi hata moja.
Azam watashuka dimbani tena leo saa 3:00 Usiku kuvaana na Tanzania Prisons.