NA MWANDISHI WETU

BAIBUI ni moja kati ya mavazi ya asili yenye kutambulisha utamaduni wa wazanzibari. Si rahisi kuthibitisha ni lini au wapi vazi hilo lilianza kuvaliwa, lakini kumbukumbu za kihistoria zinaonesha kuwa chimbuko la vazi hilo ni bara Arabu.

Kutokana na maingiliano ya wenyeji asili wa visiwa vya Unguja na Pemba kwa karne kadhaa, wahamiaji wengi kutoka Arabuni, bara Hindi na hata mataifa mengine ya Asia walifika visiwani Zanzibar kwa sababu za kibiashara hali ambayo pia ilichangia maingiliano ya kiutamaduni na kuzaliwa utamaduni mpya wa Wazanzibari.

Nadharia nyengine inadai kuwa asili ya baibui ni katika nchi ya Ajemi (Iran) ambapo wenyeji kutoka huko hasa katika mji wa Shirazi walikuwa na maingiliano na wenyeji wa visiwa vya Zanzibar tokea karne ya kumi.

Inasemekana kuwa asili ya baibui ni vazi lililovaliwa na wanawake katika ukanda mzima wa mashariki ya Kati kwa karne kadhaa kwa lengo la kustiri (kuhifadhi) mwili wa mwanamke hasa kutokana na utamaduni wa kiislamu.

Hadi leo, baibui ndilo vazi linalovaliwa zaidi na wanawake wa rika zote na ni moja kati ya vielelezo halisi vinavyotambulisha utamaduni wa visiwa vya Zanzibar.

Kwa miaka kadhaa baibui linalovaliwa visiwani Zanzibar, limekuwa likibadilika mitindo ya ushonaji na uvaaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kwenda na wakati.

Mwanzo mwa miaka ya 1900, visiwani Zanzibar kabla ya kuanza kuvaliwa “Baibui la kamba”, kulivaliwa aina fulani ya baibui lililoitwa “Lembwani”.

Lembwani ni aina fulani ya guo refu la hariri ambalo walikuwa wakivaa wanawake wenye uwezo hasa wanawake wa aila ya kisultani na wale wa kiarabu walioshi katika baadhi ya mitaa ya Mjimkongwe.

Baibui hilo la “Lembwani” lilivaliwa gubi gubi ambapo mvaaji alijifunika kuanzia kichwa hadi miguu na kubakisha sehemu ndogo ya macho ili kuona.

Baada ya kuondoka mabaibui yaitwayo “Lembwani” visiwani Zanzibar yaliingia mabaibui yaitwayo “Barkowa”. Wanawake wa Kizanzibari wakati huo, waliiga aina hiyo ya mabuibui kutoka kwa wanawake wa Oman, Kuwait na Bahrein ambao walivaa mtindo huo wa mabuibui.

Baada ya kuondoka mabaibui ya mtindo wa “Barkowa”, Wanawake wa Kizanzibari walianza kuvaa aina mpya ya baibui la kamba.

Hili ni buibui ambalo lilikuwa na kipande cha kitambaa kilichoungwa nyuma ya baibui hilo kilichokuwa na vipande viwili vya kamba ya kitambaa ambayo mvaaji huifunga kidevuni na hivyo kuacha kipande cha kitambaa kikipepea kwa nyuma.

Kipande hicho cha kamba kiliitwa “Ukaya” ambapo mvaaji anaweza kufunga kamba refu na fupi au refu zote ilitegemea kama anataka kujifunika gubi gubi, kuliachilia baibui hilo au afunge mtindo wa kizoro.

Uvaaji wa baibui uitwao “Zoro” ambao kwa sasa unaitwa “Kizoro” ulipata umaarufu visiwani Zanzibar katika miaka ya 1930 baada ya kuoneshwa mchezo wa sinema uliotwa, “The Mark of Zorro”.

Katika mchezo huo, muhusika mkuu “starring” mwenye kutumia upanga kushambulia maadui amejifunika uso wake wote kwa kitambaa na kubakisha sehemu ndogo ya macho.

Hivyo moja kwa moja, baada ya mchezo huo kuonekana katika sinema visiwani Zanzibar ndipo kina mama wakaiga na kuvaa mabaibui kwa mtindo huo wa kuficha macho.

Kwa vile wakati huo ilikuwa ni aibu kwa watoto wa kike hasa wanawari kutoka nje na kutizama ngoma, mara nyingi wari hao walivaa baibui aina ya “Kizoro” pale wanapochunguliza ngoma au maharusi.

Baadae ulikuja mchezo wa sinema uitwao “Ninja” na ndipo ukazuka uvaaji wa mabaibui uitwao “Ninja”.

Wakati mabaibui ya kamba yanaingia, kulikuwa na aina mbalimbali za vitambaa vya thamani vilivyotumika kushona mabaibui hayo.

Kutokana na tofauti ya vitambaa vilivyotumika kushona mabaibui hayo ya kamba, ndio maana pia kukawepo aina tofauti za mabaibui.

Baadhi ya mabaibui hayo ni ogri, mende, lozi, kaniki, ukoko wa halua, baibui la maua, kitina na baibui la bati. Majina hayo yalitokana na uhalisia wa aina ya kitambaa kilichotumika kushonea baibui hilo.

Baibui la bati lilikuwa likitoa sauti kama bati pale mvaaji anapokwenda, baibui la ogri lilikuwa ni jepesi na kitambaa chake laini sana ambapo baibui la ukoko wa halua kitambaa chake kilikuwa kama kina povu na kufanya aina fulani ya ukoko mweupe kama halua.

Baibui la mende kitambaa chake kilikuwa na aina fulani ya mikwaruzo kama mgongo wa mende.

Kwa wakati huo, muuzaji mkubwa wa vitambaa vya mabaibui hayo alikuwa ni mfanyabiashara aitwae Gamia aliyekuwa na duka katika mtaa wa Kiponda mjini Zanzibar karibu na “Kwa Uncle”.

Uvaaji wa baibui la kamba visiwani Zanzibar ulishamiri sana wakati wa vita vikuu vya kwanza vya dunia kati ya mwaka 1914-1918. Baadae katika miaka ya 1940, uvaaji wa mabaibui ulibadilika kutokana na mazingira.

Kwa mfano wakati huo Zanzibar ilikuwa chini ya utawala wa Sultan Seyyid Khalifa bin Haroub, ambapo mkewe Bibi Nunuu bint Ahmed alilazimika kupunguza ukubwa wa baibui lake kwa chini.

Sababu kubwa ya kupunguza baibui lake kwamba iwe rahisi kupanda kwa urahisi katika vyombo vya usafiri kama vile gari, ndege na meli. Hivyo wanawake wengi nao wakaiga mtindo wa kuvaa baibui wa Bibi Nunuu.

Baadhi ya mitindo ya uvaaji wa baibui iliyokuwa maarufu visiwani Zanzibar katika miaka ya 1940 na 1950 ni pamoja na “Kibiriti Ngoma”, ambapo mvaaji alipandisha buibui na kuliweka shingoni.

Mara nyingi mwanamke huvaa mtindo huo pale anapofikwa na jambo la dharura au hatari. Jina Kibiriti Ngoma limetokana na jina la kituo cha Polisi cha Ng’ambo ambapo zamani kikiitwa Kibiriti Ngoma.

Hivyo baibui la kamba lilimuwezesha mvaaji kujifunika au kuliachia ili watu waone aina ya nguo uliyovaa.

Kwa hivi sasa baibui la kamba ni adimu hapa Zanzibar ambapo hata vijana wengi hawalijui. Ni baadhi ya wazee wachache wanaovaa baibui hilo hadi leo.

Buibui ambalo limepata umaarufu sana visiwani Zanzibar kwa hivi sasa ni pamoja na Abaya ambalo asili yake ni bara arabu.

Kwa kawaida baibui la aina hii ambalo pia ni maarufu katika mataifa mengine ya kiislamu kama vile Iran, Indonesia na Uturuki huvaliwa na kitambaa cha kichwani kiitwacho kwa majina tofauti.

Baadhi ya majina hayo ni nikabu, hijabu, shela, burk, dupata, bushiya, buknuk, khimar, jilbab, shungi, mtandio au kilemba. Kuna baadhi ya wanawake huvaa aina hiyo ya buibui na kashda, kanga au perio.

Kuna aina mbalimbali za mabaibui ya abaya ambayo ni pamoja na abaya ya kawaida, Abaya la Bi Harusi, Ambassador Abaya, Amethyst Abaya, Artistic-tunic abaya linalonakishiwa vizuri kwa mkono na Blossom Abaya. Mabaibui yote hayo hutengenezwa kwa ukubwa tofauti kulingana na wavaaji.

Kutokana na kubadilika kwa mtindo wa kushona baibui, mabaibui mengi yanayovaliwa hivi sasa visiwani Zanzibar ni ya mitindo tofauti ambapo pia kuna baibui la Mkanda.

Hili ni baibui ambalo lina mkanda ambao mvaaji hufunga kiunoni na kukazia kwa mbele. Pia nakshi za mabuibui ya kisasa hutofautiana ingawa hadi leo bado baibui hutambulika kutokana na kuwa na rangi nyeusi.