Wananchi, wanasiasa matumaini makubwa

NA KHAMISUU ABDALLAH

WANANCHI wa Zanzibar leo wanatarajia kuipokea bajeti kuu ya serikali kwa mwaka 2021/2022 wakiwa na matumaini makubwa hasa katika masuala ya kimaendeleo.

Bajeti hiyo itakayosomwa leo jioni katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali, ikiwa ni kufuata utaratibu wa Jumuiya za Afrika Mashariki.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Uhusiano wa baraza hilo, Himidi Choko, ilisema viongozi mbali mbali wanatarajia kuhudhuria, wakiwemo mabalozi wadogo wanazoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Wakielezea matarajio yao, walipozungumza na Zanzibar Leo juu ya bajeti hiyo, baadhi ya wananchi na wasiasa, walisema wana amini kwamba uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi utazingatia maslahi ya wananchi zaidi hususani katika suala la kupunguza kodi kwa wafanyabiashara wadogo wadogo.

Mmoja wa wananchi hao, Zaitun Suleiman, alisema anatarajia bajeti hiyo itatekeleza mambo ya maendeleo waliyoahidiwa na serikali ya hasa huduma ya maji safi na salama, barabara na uboreshaji wa huduma za afya mambo ambayo bado ni changamoto kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Aidha alisema ni imani kuwa bajeti hiyo itazingatia pia mambo muhimu katika kuwawezesha wanawake na vijana katika fursa mbali mbali za ajira katika kujiajiri wenyewe.

“Tunaamini bajeti hii itatulenga sisi wananchi wanyonge kwani tuna matarajio makubwa na serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi aliahidi hatatuangusha,” alibainisha.

Nae Mfanyabiashara wa viatu, Said Seif Said, alisema wanaamini kwamba bajeti hiyo itazingatia wafayafanyabiashara katika kuwapunguzia kodi, kwani wafanyabiashara wengi ni wachanga na hawana uwezo wa kuchukua mikopo mikubwa.

Alisema kipindi cha kampeni Rais Mwinyi aliwaahidi mambo mengi ikiwemo suala la kuwapunguzia kodi jambo ambalo wanaamini katika bajeti hiyo litawapa matumaini makubwa.

Salum Issa alisema wafanyakazi wa serikali wana imani kubwa na bajeti yao hasa suala la maslahi bora na vitendea kazi ili kuwapa ari ya kufanya kazi hasa katika kuwahudumia wananchi kupitia tasisi mbalimbali.

Nae Mwenyekiti wa chama cha ADA TADEA, Juma Ali Khatib, alisema anaamini kwamba bajeti hiyo imelenga kuwasaidia wananchi na kwenda katika uchumi wa buluu ikiwemo masuala ya wavuvi, rasilimali ya gesi na mafuta na ufugaji wa samaki kilimo yatazingatiwa kwa kiasi kikubwa.

Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuongoza nchi vizuri hadi kufikia kipindi hichi kwani amefanya mambo makubwa na juhudi kubwa katika kuzuia mianya wizi, upotevu wa fedha za wananchi, rushwa na uzembe.

“Wananchi wengi wa Unguja na Pemba wamekuwa na imani na kiongozi wao katika utendaji wake wa kazi ambayo dhamira yake kubwa ya kuleta manufaa kwa watu wanyoge, wafanyabiashara, wakulima na wafugaji,” alieleza Khatib.

Kwa upande wake, Katibu wa Kamati Maalum Idara ya NEC, Itikadi na Uenezi Zanzibar, Catherine Peter Nao, alisema matarajio yake ni kuona bajeti hiyo itakuwa na mambo mazuri katika meneo yote na kuamini serikali ya awamu ya nane itakuwa imejipanga na kujidhatiti katika maeneo muhimu.

Akizungumzia utekelezaji wa ilani alisema anaamini bajeti hiyo itagusa ilani ya CCM kwa mwaka 2020/2025 kwani ndio inayobeba bajeti nzima kwani ndio yenye mkataba baina ya serikali na wananchi.

Alibainisha kuwa ni imani kwamba maeneo muhimu ikiwemo ajira zilizotamkwa katika ilani ni kuona sasa njia gani zitapatikana na hata ujenzi wa viwanda, ujenzi wa barabara za ndani na barabara kuu na suala la maji safi na salama.

Hivyo, aliwaomba wananchi kuhakikisha wanaisikiliza bajeti yao na kuona muelekeo wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane katika mambo ya kimaendeleo.