NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

WANANCHI wa kata ya Sokoni jijini Arusha, huenda wakaondokana na adha ya muda mrefu ya ubovu wa barabara baada ya halmashauri ya jiji la Arusha kupitia diwani wa kata hiyo kuanza kuzifanyia matengenezo barabara korofi zilizoathiriwa na mvua pamoja na ujenzi wa Mradi wa Bomba la maji taka.

Hatua hiyo pia itawanufaisha wananchi wa kata zingine za jiji hilo wenye shida kama hiyo ya ubovu wa barabara .

Wakiongea wakati wa zoezi la kumwaga vifusi vya Moramu kwenye barabara korofi baadhi ya wananchi wa kata hiyo ,Iddy Msangi, Mariam Issa na Nyasu Fundikira, wameishukuru Serikali kupitia diwani wao Salun Olodi kwa hatua hiyo na kutaka jitihada zaidi zifanyike, ili kuwaondolea adha hiyo iliyowakumba kwa muda mrefu ya barabara kutopitika

“Sisi Wakazi wa mtaa wa Lolovono tunateseka Sana barabara yetu ya jumba Bibi imeharibika Sana na mvua pamoja na mkandarasi aliyekuwa akichimbia mabomba ya maji taka kwa sasa hakuna gari inayopita huku tunaomba Serikali iongeze jitihada za kuzifanyia matengenezo ikiwemo mitaro”alisema Mariam Issa ambaye nibalozi wa mtaa huo.

Naye diwani wa kata ya Sokoni, Salun Olodi ,amemshukuru Mkurugenzi na Meya wa jiji la Arusha, baada ya kuona umuhimu wa kuzifanyia matengenezo barabara korofi katika kata yake na kata nyengine za jiji la Arusha.

Olodi amesema ni wakati mwafaka wa kuwatumikia wananchi, ili kuwaondolea adha hiyo ya muda mrefu ambapo barabara nyingi za kata ya Sokoni ,zimeharibiwa vibaya na mvua, hatua iliyosababisha wananchi kutembea kwa miguu umbali mrefu kufuata huduma muhimu za kijamii baada ya magari ya abiria kutofika maeneo hayo.

“Mkakati wangu Ni kuhakikisha napunguza changamoto hii ya ubovu wa barabara katika kata yangu ya Sokoni 1 “amesema.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Lolovono, Olgenance Lema, katika kata ya Sokoni, amemshukuru diwani wa kata hiyo kwa jitihada zake zilizofanikisha kuanza kwa matengenezo ya barabara na hivyo kupunguza adha kwa Wananchi.