HIVI karibuni kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un alitoa taarifa yenye ujumbe mkali dhidi ya taifa hasimu kwa nchi hiyo Marekani.

Kim alipeleka ujumbe wa moja kwa moja kwa utawala wa Joe Biden ambapo aliamuru nchi yake kuwa tayari kwa mambo mawili mazungumzo na makabiliano dhidi ya Marekani.

Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini (KCNA), liliripoti kuwa kauli ya kiongozi huyo imekuja chache baada ya Marekani na mataifa mengine kuihimiza nchi hiyo kuachana na mpango wake wa nyuklia na kurudi kwenye mazungumzo.

Baadhi ya wataalamu wanasema kauli ya Kim inaonesha kuwa ana uwezekano wa kushinikiza kuimarisha silaha zake za nyuklia na kuongeza shinikizo kwa Marekani kuachana na kile ambacho Korea Kaskazini inazingatia kuwa sera ya uhasama kwa nchi hiyo, ijapokuwa pia ataandaa kuanza tena kwa mazungumzo.

Wakati wa mkutano uliokuwa ukiendelea hivi karibuni wa chama nchini Korea Kaskazini, Kim alichambua kwa makini muelekeo wa sera za Marekani chini ya rais wa nchi hiyo Joe Biden na kufafanua hatua za kuchukuwa katika uhusiano na Marekani.

Mnamo mwaka 2018, Kim alishiriki mazungumzo mara kadhaa na aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu hatua ya Korea Kaskazini na miradi yake ya silaha za nyuklia.

Lakini mazungumzo hayo yalisambaratika baada ya Trump kukataa wito wa Kim wa kuondolewa kwa vikwazo vikali ili aweze kuachana na sehemu ya mpango wake wa nyuklia.

Utawala wa Biden umeanzisha mbinu mpya ya kufuatilia mpango wa nyuklia wa Korea Kasakzini ambayo imeitaka kuwa iliyosawazishwa na inayoweza kutumika.

Maelezo kuhusu mbinu hiyo hayajachapishwa lakini maofisa wa Marekani wamependekeza kuwa Biden atatafuta usawa kati ya mikutano ya moja kwa moja kati ya Kim na Trump na uvumilivu wa kimkakati wa aliyekuwa rais, Barack Obama, katika kukabiliana na mpango wa nyuklia wa Kim.

Hivi karibuni katika kikao chao viongozi wa kundi la mataifa saba yenye ushawishi zaidi duniani, G7, walitoa taarifa ya kutaka kusitishwa kabisa kwa mpango wa nyuklia na mipango ya makombora katika rasi ya Korea. Viongozi hao walitoa wito kwa Korea Kaskazini kurudi tena katika mazungumzo.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema mjumbe wake kuhusu Korea Kaskazini, Sung Kim, anatarajiwa kufanya ziara nchini Korea kwa mkutano wa mataifa matatu na maofisa wa Korea Kusini na Japan.

Ziara hiyo inasisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pande hizo tatu katika kuhakikisha kukatizwa kwa mpango wa nyuklia katika rasi ya Korea.

Taarifa za karibuni zinaeleza kuwa mjumbe maalumu wa Marekani kwa Korea Kaskazini anatumai kupata jibu la kuridhisha kutoka kwa taifa hilo, baada ya Marekani kupendekeza wafanye mazungumzo wakati wa safari yake ya mjini Seoul.

Sung Kim, mwakilishi maalumu wa Biden kwa Korea Kaskazini, alifanya ziara mjini Seoul kwa mazungumzo na maofisa wa Korea Kusini na Japan kuhusu uhusiano unaosuasua kati ya Korea Kaskazini na Marekani kutokana na mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini uliopelekea Marekani kuiwekea nchi hiyo vikwazo.

Baada ya kukutana na Noh Kyu-duk, mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa Korea Kusini, mjumbe maalumu wa Marekani Sung Kim alisema washirika wake wamesikiliza vyema matamshi ya kiongozi huyo wa Korea Kaskazini aliyoyatoa hivi karibuni na matumaini yao ni kwamba atakubali kufanya mazungumzo na Marekani hivi karibuni.

Sung Kim aliwaambia waandishi wa habari kwamba Korea Kusini na Marekani wataendelea kuwa na ushirikiano wa karibu ili kuimarisha hali katika rasi ya Korea na kutafuta njia ya kuanza tena mazungumzo na Korea Kaskazini haraka iwezekanavyo.

Kurudi nyuma kwa maendeleo ya kiuchumi ya Korea Kaskazini kulitokana na kuharibika kwa mazungumzo kati ya Kim Jong Un na Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump mwaka 2019, baada ya kiongozi huyo wa Korea Kaskazini kutaka nchi yake iondolewe vikwazo vya kiuchumi ili naye apunguzi baadhi ya shughuli zake za kinyuklia.

Katika hotuba zake za hivi karibuni, Kim Jong Un ametishia kuimarisha silaha zake za nyuklia na kudai kuwa hatima ya diplomasia na uhusiano wa nchi hizo mbili inategemea ikiwa Marekani itakubali kuaachana na kile alichokieleza kama sera za uhasama.

Maofisa wa Marekani wamesema kwamba Biden atakuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Kim kama alivyofanya Trump, lakini pia atatumia busara ya Barack Obama ya kuwa na ustahmilivu.

Lakini baadi ya wachambuzi wanasema Korea Kaskazini italazimika kuchukua hatua za kweli za kupunguza shughuli zake za kinyuklia kabla ya Biden kukubali kuiondoshea vikwazo ilivyowekewa na Marekani.

Nchini China, msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Zhao Lijiang, alitoa wito wa kurejelewa kwa mazungumzo kati ya Korea kaskazini na Marekani na kusema kuwa wanaamini rasi ya Korea inakabiliwa na awamu mpya ya mvutano.