NA HASHIM KASSIM

MWENYEKITI wa bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba SC Mohammed Dewji ‘Mo’ ameahidi ushirikiano na mabigwa wa ligi kuu soka visiwani Zanzibar KMKM.

Ahadi hiyo aliitoa wakati alipoitembelea timu hiyo kwenye Ofisi zao Maisara, na kusema wako tayari kusaidiana na timu hiyo kwenye sekta mbalimbali.

Mo alieleza kuwa watajitahiji kusaidiana kwa hali na mali na mabingwa hao kwa lengo la kuhakikisha michezo hasa soka inapata maendeleo pamoja na kuwaalika KMKM kwa mchezo wa kirafiki na Simba SC.

“Tunajua kuna vijana munataka kuleta kwetu munaweza, karibuni kucheza na sisi na kama tuna sehemu ya makocha ambao wanaweza kuwasaidia tutawapa kwa lengo la kujenga uhusiano na pia tutaisaidia klabu” Alisema Mo Dewji.

Kwa upande wa sports ofisa wa klabu ya KMKM Fc Ali Shein alisema ujio wa mwekezaji huo mkubwa barani Afrika ni faraja kwao na wanamatarajio mazuri kutoka kwa Mo.

“Ugeni huu ni mkubwa sana kwetu kuja kututembelea klabuni na kimichezo tunatarajia mazuri kutoka kwake, ijapokuwa hajatwambia katuandalia nini ila matajio yetu ni makubwa” Aliongezea Shein.

Ujio wa mwekezaji huyo klabuni hapo ni utekelezaji wa ahadi ya mkuu wa kikosi cha KMKM Commodore Azanna Hassan Msingiri aliyoitoa wakati akiwakabidhi kombe la ligi kuu soka Zanzibar timu hiyo katika uwanja wa Amani.