NA MWINYIMVUA NZUKWI

SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid, amewahimiza wajumbe wa baraza hilo kuhakikisha wanaifahamu mifumo ya upatikanaji wa fedha na rasilimali nyengine kutoka kwa washirika wa maendeleo ili kuchochea kasi ya maendeleo endelevu ya Zanzibar na watu wake.

Aliyasema hayo jana wakati akifungua warsha ya siku moja kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi juu ya muongozo wa mashirikiano ya utafutaji rasilimali fedha na mikopo kwa miradi ya maendeleo iliyofanyika katika ukumbi wa baraza hilo Chukwani, zanzibar.

Zubeir alisema, baraza la wawakilishi kikiwa chombo cha kinachoisimamia serikali hivyo ipo haja kwa wajumbe wake kuwa na uelewa wa kutosha juu ya mifumo na miongozo inayotumika kupata fedha.

Aliwataka wajumbe hao kufuatilia kwa kina mafunzo hayo ili yawasaidie katika utekelezaji wa majukumu yao kitaalamu na kuleta ufanisi zaidi.

“Warsha hii imekuja katika wakati muafaka hivyo ni rai yangu kuhakikisha tunazingatia na tunafahamu kikamilifu ili iwe rahisi kuisaidia na kuisimamia serikali kwenye utekelezaji wa mipango na miradi iliyojipangia,” alisisitiza Spika Zubeir.

Aliongeza kuwa wajumbe wana wajibu wa kuisimamia serikali kwa kuzingatia mwelekeo wa mipango ya kitaifa, kimataifa na bajeti lakini pia kusaidia kuibua miradi yenye tija.

Wakizungumza kando ya warsha hiyo, wajumbe wa baraza hilo Ali Suleiman Mrembo na Sabiha Filfil Thani, walieleza kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutambua namna mipango ya serikali inavyoandaliwa pamoja na kupatiwa fedha za utekelezaji.

Walisema, ipo haja ya kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa rasilimali fedha lakini pia kuwafanya wawe na uelewa wa kuibua miradi itakayowasaidia wananchi wao.

“Tumepata kujua namna ya fedha za washirika wa maendeleo zinavyopatikana lakini pia wadau wanaochangia utekelezaji wa mipango na mikakati yetu kama nchi,” alisema Mrembo.

Aliongeza haja ya washirika hao kutoa fedha kwa wakati kwenye miradi iliyokubaliwa lakini pia watekelezaji wa miradi hiyo kuwa na usimamizi mzuri wa fedha hizo ili tija ipatikane.

Awali akiwasilisha mada bya mwongozoo wa mashirikiano kati ya serikali na washirika wa maendeleo, afisa mwandamizi kutoka idara ya fedha za nje katika Afisi ya Rais, Fedha na Mipango,  alieleza kuwa mwongozo huo unaweka utaratibu wa majadiliano kati ya serikali na wadau wa maendeleo ili kupata fedha kwa njia ya mikopo, ruzuku au misaada ya kibajeti.

Alieleza kwamba kupitia mwongozo huo imepalekea kupatikana kwa ubora wa utekelezaji wa miradi inayopatiwa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo ja,mbo linalochochea maendeleo ya nchi.

Nae Ramadhan Khamis Sosela, kutoka Tume ya mipango Zanzibar, akiwasilisha mwongozo wa utafutaji rasilimali fedha, ruzuku na mikopo kwa miradi ya maendeleo, alihimiza haja ya miradi inayoandaliwa na sekta au taasisi za seriklai kupitia kwa makatibu wakuu kwani wao ndio wasimamizi wakati wa utekelezaji.

Mapema akimkaribisha Spika kufungua warsha hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya nchi Afisi ya Rais, Fedha na Mipango kupitia Idara ya fedha za nje, Waziri wa wizara hiyo, Jamal Kassim Ali, alieleza kuwa hatua imelenga kujenga uelewa wa wajumbe juu ya maswala ya miradi na upatikanaji wa fedha za utekelezaji wake.

Alieleza kuwa kwa kipindi kirefu jamii ya kimataia, kikanda na asasi za kiraia za ndani na nje ya nchi zimekuwa zikifadhili na kusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo nchini hivyo kuna umuhimu mkubwa kwa wajumbe hao kuzifahamu taratibu hizo.