NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

BENKI Kuu ya Tanzania (BOT), imewasajili watoa Huduma Ndogo za Fedha wa daraja la pili 446 katika mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara hadi kufikia mwezi Mei, 31 mwaka huu.

Gavana wa BOT, Prof. Florens Luoga,  akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, amesema orodha hiyo imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.

Alisema watoa huduma hao wamesajiliwa kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma, Njombe, Kagera, Tabora, Songwe, Iringa, Shinyanga na mikoa mengine ya Tanzania Bara, ambao wamewasilisha maombi ya leseni Benki Kuu ya Tanzania.

Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 57 cha sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha ya mwaka 2018, watoa huduma wa Daraja la Pili ambao hawakuwasilisha maombi ya leseni BOT kabla ya Aprili 30 mwaka huu, hawapaswi kuendelea kufanya biashara ya huduma ndogo za fedha hadi wawe wamepata leseni.

Allieleza kuendelea kufanya biashara bila kuwa na leseni ya Benki Kuu ni uvunjifu wa sheria unaoweza kupelekea faini au kifungo kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.

Aidha alisema BOT itaendelea kutoa machapisho ya orodha iliyohusishwa na watoa huduma ndogo za fedha wa daraja la pili waliosajiliwa, ikiwemo orodha ya watoa huduma ndogo wa daraja la tatu na la nne.