NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Florens Luoga amesema muda wa mwisho wa usajili wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha (VIKOBA), Novemba 30, mwaka huu.

Awali zoezi la usajili lilikuwa likamilike mwezi Aprili 30, mwaka huu lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza katika usajili, muda huo umeongezwa hadi Novemba 30 mwaka huu, ambapo muda huo wa ziada hauhusu watoa huduma ndogo za fedha wa daraja la pili wala la tatu.

Akitoa taarifa hiyo jana, kwa vyombo vya habari, amesema kutokana na changamoto zilizojitokeza katika usajili wa vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha, kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ameridhia kuongeza muda wa miezi sita zaidi kwa ajili ya usajili wa vikundi hivyo.

Alisema mwezi Disemba 2019, BOT ilitoa taarifa kwa umma kuhusu sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha ya mwaka 2018 iliyoanza kutumika rasmi Novemba 1, 2019.

Aidha alieleza pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo ilirejea kifungu cha 57 cha sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ambacho kinawataka watoa huduma ndogo za fedha wote kuwasilisha maombi ya leseni ya usajili BOT au kwenye Mamlaka kuwasilishwa katika kipindi cha miezi 12 baada ya sheria kuanza kutumika Oktoba 31, mwaka jana.

BOT inatarajia kuwa vikundi hivyo vitatumia vizuri muda wa ziada kukamilisha na kuwasilisha maombi ya usajili kwa njia ya kielektroniki, ambapo vikundi vitakavyopata changamoto yoyote katika kuwasilisha maombi hayo vinashauriwa kuwasiliana na Maafisa Maendeleo ya Jamii au Maafisa TEHAMA katika Halmashauri iliyo karibu nayo.

Alisema BOT, inaendelea kuutahadharisha umma kuhusu matangazo na maelekezo yenye kupotosha na kuleta taharuki yanayotolewa na watu wasiokuwa na nia njema kuhusu dhamana na madhumuni ya usajili wa watoa huduma ndogo za fedha, badala yake wananchi wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka husika.