TAIFA la Zambia limethibitisha kifo cha mzee Kenneth Kaunda, ambaye kabla ya kifo hicho siku chache zilizopita alikimbizwa hospitali kutokana na afya yake kuzorota 

Mzee Kaunda kwa hakika alikuwa ni mmoja wa viongozi waasisi wa Afrika mpya, na alichukua madaraka mara baada ya Zambia kufanikiwa kupata uhuru kutoka kwa wakoloni wa kiingereza.

Jina lake hasa ni Kenneth David Kaunda alizaliwa Aprili 28 mwaka 1924 katika kituo cha wamishonari karibu na mpaka baina ya Rhodesia Kaskazini (Zambia ya sasa) na Congo, ambapo hadi anafariki Juni 17 mwaka 2021 alikuwa na umri wa miaka 97.

Kabla ya kifo chake Juni 14 mwaka huu alikimbizwa hospitalini mjini Lusaka akikabiliwa na ugonjwa niumonia, ambapo alifariki siku tatu baadae na serikali kutangaza siku 21 za msiba wa kitaifa kuomboleza kifo cha kiongozi huyo aliyepigania uhuru wa taifa.

Wakati wa miaka ya mwisho wa uhai wake, Kenneth Kaunda na mke wake waliishi maisha ya kawaida kabisa katika mji mkuu, Lusaka.

Baba yake, alikuwa mchungaji aliyetawazwa na kanisa la Uskochi ‘Church of Scotland’, alifariki alipokuwa bado mtoto na kuiacha familia katika hali ya dhiki ya umasikini.

Hata hivyo, uwezo wake mkubwa wa kielimu ulimpatia fursa katika skuli ya kwanza ya sekondari iliyoanzishwa kaskazini mwa Rhodesia na baadaye akawa mwalimu.

Kazi hiyo aliifanya katika jimbo la Copperbelt na Rhodesia Kusini, ambayo kwa sasa ni Zimbabwe, ambako kwa mara ya kwanza alipata uzoefu na kuchukizwa sana na athari za utawala wa wazungu.

Moja ya vitendo yake ya kisiasa ilikuwa ni kuto kula nyama kama njia ya kupinga sera ambayo iliwalazimisha Waafrika kwenda kwenye dirisha lililotengwa kwa ajili yao kwenye vichinjio vya kununua nyama.

Mwaka 1953 alikuwa katibu mkuu wa vuguvugu la Northern Rhodesian African National Congress, lakini vuguvugu hilo lilishindwa kuwahamasisha Waafrika dhidi ya shirikisho tawala la wazungu la Federation of Rhodesia na Nyasaland.

Miaka miwili baadaye alifungwa jela na kukabiliwa na adhabu kali, kwa kusambaza vijikaratasi ambavyo mamlaka ilioviona kama uchochezi dhidi ya utawala wa kikoloni.

Kwa kukata tamaa na kile alichokiona kama kushindwa kwa chama chake kuchukua msimamo mkali wa haki za wazawa Waafrika, Kaunda alianzisha chama chake cha Zambian African National Congress.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, kilipigwa marufuku na Kaunda alirejeshwa tena gerezani kufungwa kwake kulimfanya ageuke kuwa mkali.