MWANDISHI WETU, TANGA

CHAMA Cha Mapinduzi kimesisitiza kuwa kitaendelea kutoa mwelekeo wa siasa na uongozi wa nchi kwa vile ndicho kinachounda na kuongoza serikali.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na wazee wa wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, wakati wa ziara ya watendaji wakuu wa sekretarieti ya chama hicho mkoani humo jana.

Alisema viongozi wa chama katika ngazi zote wana jukumu la kufuatilia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2020-2025 katika kufuatilia na kuondoa kero na changamoto za wananchi pamoja na kuharakisha maendeleo.

Alisema CCMina dhamira ya kutoshiriki siasa za kuhamasisha vurugu badala yake kitandelea kuhimiza siasa safi zinazojali ustawi wa haki, usawa, amani, usalama, umoja na mshikamano na kusimamia maslahi ya wananchi walio wengi.

Alisema baadhi ya matamko ya viongozi vyama vya upinzani hayana afya katika ujenzi wa umoja wa kitaifa hasa kipindi hiki ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amejipambanua katika kuwatumikia Watanzania bila kuwabagua kwa misingi ya itikadi zao za kisiasa, ukanda, ukabila na udini.

“Matamshi yaliyotamkwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa hivi karibuni yamevuka mipaka. Yamewathibitishia Watanzania kuwa baadhi ya vyama hivyo havina wanasiasa wenye maarifa na upeo wa kutambua dhana ya mgawanyo wa madaraka,” alieleza Shaka.

Aidha Shaka alifafanua kuwa hakuna chama chochote cha siasa chenye wajibu wala haki ya kumuamrisha Rais wa nchi ambae pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama au kutoa shinikizo katika maamuzi ya Rais hususani juu ya muda, wa kuwaona wananchi ndani ya nchi anayoiongoza.

“Hakuna sababu ya kutishana wala kutoa masharti na mashinikizo kwa jambo lolote lile kwani ni Rais Samia kwa kuthamini kwake ushirikishwaji wa kila mmoja wetu katika ujenzi wa nchi yetu,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa ipo haja ya wanansiasa hao kumuacha rais kutekeleza majukumu yake na akiona inafaa kukutana na vyama vya siasa ataamua ni wakati gani akutane nao.

Shaka yuko katika ziara ya kikazi mkoani Tanga ambapo ataendelea na ziara yake katika Wilaya ya Tanga mjini, ziara hiyo inaongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo ambaye amefanya ziara wilaya za Kilindi, Handeni na Korogwe.

Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu aliongozana pia na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Mstaafu Ndugu Ngemela Lubinga ambaye anapita wilaya za Mkinga, Lushoto na Bumbuli.