NA KHAMISUU ABDALLAH
MKUU wa KMKM Commodore Azana Hassan Msingiri, amesema anakusudia kukiondoa katika utegemezi kutoka serikalini kwa kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali itakayokifanya kujitegemee kiuendeshaji.
Kauli hiyo alitoa Makao Makuu ya KMKM Kibweni wakati akizungumza na Mwekezaji Mohammed Dewji na ujumbe wake kutoka Dar es Salam waliofika kwa lengo la kuwekeza katika kikosi hicho.
Alisema lengo kubwa la kikosi hicho ni kuzalisha katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya bahari ikiwa ni mikakati ya kuiunga mkono serikali inayoongozwa na Dk. Hussein Mwinyi kwenye utekelezaji wa sera wa uchumi wa buluu.
Aidha alisema lengo hilo ni kwenda sambamba na sera ya uchumi wa buluu kwa vitendo kwani kikosi hicho kimejipanga na kuanza taratibu za uvuvi wa maji madogo hadi bahari kuu.
Hata hivyo alimuelezea Mwekezaji huyo kuwa KMKM kina miradi mingi ya ujenzi kwa sasa ikiiwemo mradi wa kujenga chelezo ambacho hadi sasa wameshafanya utafuti wa mwanzo.
Commodore Misingiri alibainisha kuwa mwaka huu serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewapatia bilioni 62 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huo na mpango huo utakuwa kwa muda wa miaka mitatu.
Hata hivyo alibainisha kuwa KMKM pia ina eneo la kujenga hoteli kubwa ya kitalii katika eneo la karibu ya Kambi ya KMKM eneo ambalo halipungui hekta zaidi ya 15.
Hivyo alimkaribisha Mwekezaji huyo kuekeza katika eneo hilo au kutafuta mtu ataekuwa sahihi kuekeza kwani Mkoa huo ndio maarufu kwa ajili ya shughuli za kiutalii katika visiwa vya Zanzibar kuliko Mikoa mengine.
Alisema miongoni mwa malengo ya baadae ni kununua meli kwa ajili ya kusafirisha abiria katika bahari ya hindi, lakini pia kusafirisha mizigo baina ya visiwa vya Pemba na Unguja.
Nae, Mohammed Deuji ameahidi kuchukua maombi na mawazo ya Mkuu wa Kikosi hicho na kuyafanyia kazi kwa haraka hasa katika sekta ya uwekezaji.
Aidha Dewji alisema katika uwekezaji wake si lazima aekeze katika kujenga viwanda ila anaweza kueka uwekezaji wake hata kwa kutoa pesa ili kuchangia mradi katika mradi husika
Akizungumzia kuhusu kuekeza katika kampuni ya ujenzi ya KMKM alisema yupo tayari kusaidia katika maeneo yenye changamoto ili waweze kutimiza malengo yao katika kuinua uchumi wa nchi na wananchi wake.