NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Suzan Peter Kunambi, amezitaka shehia nne za jimbo la Welezo   zilizoanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi kutekeleza vyema dhana ya polisi jamii kupunguza vitendo vya uhalifu.

Akizungumza vijana wa polisi jamii  wa shehia ya  Munduli wakati wa hafla ya uzinduzi na kukabidhi vitambulisho vya polisi jamii,  Suzan alisema   ipo haja ya jamii kushirikiana kukomesha vitendo uporaji na matumizi ya dawa za kulevya  vinavyojitokeza katika maeneo yao hususan wakati wa usiku.

Alisema kwa muda mrefu wananchi na watumiaji wa njia hiyo wamekuwa wakikabwa, kuporwa na kuibiwa mali zao, jambo ambalo linapaswa kudhibitiwa.

Hivyo aliwataka vijana waliojitolea kufanya kazi ya ulinzi kuwa waadilifu na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na miongozo watakayopatiwa na jeshi la polisi.

“Matendo ya uhalifu katika maeneo haya yamekuwa kero kubwa sio kwa wakaazi pekee bali pia wapita njia hususani wakati wa usiku, lazima tuungane kukomesha” alisema Suzan.

Hivyo alieleza kuwepo kwa vikundi hivyo kutapunguza na kuondosha vigenge kwa vijana wanaouuza na kutumia dawa za kulevya ikiwemo bangi na kuwapongeza vijana hao kwa uamuzi wao huo.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa wilaya amezishukuru familia tano zilizohamishwa kwenye makaazi yao katika eneo la Mtoni Chemchem kutokana na kuwa katika eneo hatarishi kwa ustahamivu na kukubali kuyahama makaazi hayo.

Suzan alitoa shukrani hizo ofisini kwake, Mwera baada ya kushuhudia zoezi la ugawaji wa fedha kwa ajili ya kodi kwa kipindi cha miezi mitatu wakati serikali ikitafuta njia za kuwapatia wakaazi hao makaazi ya kudumu.

Aidha Suzan aliwanasihi wananchi hao kutorejesha familia zao katika makaazi hayo badala yake watumie fedha walizopatiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Tunapowarudishia funguo, hatuna maana mwende mkarejee kwenye nyumba zenu kwani  lile eneo bado hatarishi ndio maana serikali ikaamua kuwahamisha,” alisema Suzan.

Akikabidhi fedha hizo, Mkurugenzi Mkuu kitengo cha operesheni na huduma za jamii, Haji Faki Hamad, aliwataka wananchi hao kupokea fedha hizo ingawa hazikidhi mahitaji waliyonayo.

Alieleza kuwa pamoja na uchache wake, fedha hizo zitawasaidia katika kipindi hiki kigumu kwa vile wananchi hao kwa sasa wamekodi baada ya kuhamishwa katika makaazi yao ya awali.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wenzake, Juma Haji Juma, aliishukuru serikali kuu na ya wilaya kwa kuonesha kuwajali na kuomba kupatiwa makaazi ya kudumu baada ya kuisha kwa kukodi.

Makabidhiano ya fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Mohammed, wakati alipofanya ziara wilayani humo miezi michache iliyopita.

Katika ziara hiuyo, Hemed aliagiza wananchi hao wahamishwe na kuwaahidi kuwasaidia fedha za kodi, ili waweze kuendelea na shughuli nyengine za kujitafutia kipato.