NA ASYA HASSAN

MKUU wa Wilaya ya Kati,  Marina  Joel Thomas, amewataka wavuvi kufuata taratibu na sheria za nchi, ili kujiepusha na migongano isiokua ya lazima.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wavuvi wa shehia tano za Uroa, Pongwe, Marumbi, Ukongoroni na Charawe katika ziara ilioambatana na wakurungenzi na maofisa kutoka Idara ya Uvuvi na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya hiyo.

Alisema kumekuwa na baadhi ya wavuvi kutumia vifaa vya kuvulia ambavyo vimepigwa marufuku na serikali jambo ambalo linapelekea kuharibu mazingira na mazalio ya samaki.

Marina alisema kufanya hivyo kunasababisha kurejesha nyuma jitihada na malengo ya serikali katika kuimarisha uchumi wa buluu.

Hata hivyo, alifahamisha kwamba serikali ya Wilaya kupitia ujumbe huo haipendezwi kuona mambo hayo yanaendelea hivyo aliwataka  wavuvi hao kutoa ushirikiano katika kuyalinda mazingira ya bahari na viumbe vyake kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.

Mkurungenzi kutoka Idara ya Hifadhi ya maeneo ya bahari Dk. Makame Omar Makame, na Mkurugenzi kutoka Idara ya Uvuvi na mazao ya Baharini Salim Sudi Hamed, walisema serikali kupitia wizara ya uchumi wa buluu inalengo la kuwawezesha wananchi kupitia mazao na rasilimali za bahari ili kuweza kukidhi kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Akiyataja miongoni mwa rasilimali hizo alisema ni pamoja na ufugaji wa nyuki na ufugaji wa kaa kwa kutumia rasilimali ya mikoko hivyo ni vyema kutoa ushirikiano wa kutoharibu mazingira hayo ili azma hiyo iweze kufikiwa.

Nae msimamizi mratibu maeneo ya hifadhi za bahari, Omar Hakim Foum na Mwanasheria wa Idara hiyo, Mwinyi Matata Mwinyi, walitumia fursa hiyo kuwataka wavuvi hao kuacha na kutumia vifaa visivyo halali ikiwemo uvuvi wa kukokota jambo ambalo husababisha kuharibu mazalia ya samaki.

“Kufanya hivyo ni kwenda kinyume na taratibu na sheria za nchi kutokana na kuharibika kwa matumbawe ambayo huchukua muda mrefu kuyarejesha,”alisema.