NA MARYAM HASSAN

DEREVA wa basi aina ya ‘Coster’ amenusurika kwenda rumande, baada ya kukamilisha masharti aliyopewa na Hakimu wa mahakama ya wilaya Mwera, Hamad Mohammed Ngwali, dhidi ya shitaka la kusababisha ajali na kumsababishia maumivu ya kiuno dereva mwenzake.

Mustafa Iddi Haji (48) mkaazi wa Muungoni, amejinusuru kwenda rumande baada ya kusaini bondi ya shilingi 1,000,000 pamoja na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao walimdhamini kwa kusaini bondi ya kima hicho hicho cha fedha, huku wakiwasilisha kopi ya vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi na barua za Sheha wa Shehiya wanazoishi.

Kabla ya kutolewa kwa masharti hayo ya dhamana, mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kesi ya kuendesha chombo cha moto barabarani bila ya hadhari na kusababisha ajali.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 24 mwaka jana majira ya saa 6:00 za mchana, huko Muungoni wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.

Siku hiyo akiwa dereva wa gari ya abiria yenye nambari za usajili 796 HM iyendayo njia namba 310 aina ya Coster, akitokea upande wa Kitogani kuelekea Muyuni, aliendesha gari hiyo bila ya hadhari na uangalifu na matokeo yake aliigonga gari yenye nambari za usajili Z 226 JY aina ya Fuso.

Gari hiyo, ilikuwa ikiendeshwa na Fadhil Ali Makame aliyekuwa akitokea Kitogani kuelekea Muyuni na kumsababisha maumivu katika kiuno chake, jambo ambalo ni kosa kisheria.