NA IS-HAKA OMAR

VIONGOZI na watendaji wa Chama cha Mapinduzi wametakiwa kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.

Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Mabodi, katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM katika wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Alisema endapo viongozi hao wa ngazi mbalimbali watakagua miradi inayotekelezwa na serikali itakuwa ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo maelekezo yaliyotolewa katika ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.

Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kutoridhishwa na maelezo yaliyotolewa na meneja wa mradi wa ujenzi wa gati ya bandari ya Mkokotoni.

Alisema maelezo yaliyotolewa na meneja huyo hayafanani na maelezo aliyopatiwa na Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi huo wa gati hiyo uliopo mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema maelezo yaliyotolewa na meneja huyo Jafar Majilanga ni kinyume na maagizo yaliyotolewa kwa Makamu wa Pili wa Rais ambapo ujenzi huo ulitakiwa kuongezwa gati ya bandari hiyo mita 120.

Alieleza kuwa maelezo aliyopewa Makamu huyo wa Pili wa Rais wamekubaliana kuchimba kuongeza kina cha maji cha bahari kwa kufikia mita 120 hata hivyo hadi sasa tayari wamefikia mita 70 na anatarajia kuongeza mita 30 ili wachimbe kwa lengo la kufikia mita 100 ndipo waanze kazi ya kuchimba.

Aidha alisema CCM imedhamiria kutekeleza kwa vitendo ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kasi ya aina yake na kwamba amewataka wanachama wa CCM kutolaza damu na badala yake wajue kuwa muda huu ndio muda wa kushuka chini kwa wananchi kusimamia utekelezaji huo wa ilani.

Wakati huo huo Naibu Katibu Mkuu huyo alipotembelea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji wa kilimo cha mpunga bonde la Kibokwa aliwataka wakulima wa kilimo cha mpunga kutambua kuwa CCM itawanufaisha kupitia sera, ilani ya uchaguzi ya CCM.

Kwa upande wake Meneja wa mradi wa ujenzi wa bandari ya Mkokotoni Jafar Majilanga alisema mradi huo unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 6.4 huku shilingi bilioni 2.2 tayari zishatumika.

Alisema mradi huo ulianza Juni 8 mwaka huu na unatarajiwa kumalizika Septemba 21 mwaka huu huku ukikamilika kwa asilimia 50 na katika ujenzi huo wa gati katika bandari hiyo rasilimali zinazotumika kwenye mradi ni mawe na nondo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Umwagiliaji kutoka Wizara ya Kilimo Umwagiliaji na Mifugo, Haji Hamid Saleh, alisema mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji wa kilimo cha mpunga cha Kibokwa utasaidia kukuza uzalishaji wa chakula na kwamba unatarajiwa kuwanufaisha wakulima 15,000 wa eneo hilo.