NA ASYA HASSAN

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, amesitisha kwa muda shughuli za kuponda kokoto katika viwanda vya matofali hadi pale serikali itakapotoa muongozo wa uendeshaji wa shughuli hizo.

Dk. Mkuya alieleza hayo kwa nyakati tofauti maeneo ya Bumbwini na Mangapwani, wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, alipokuwa katika ziara ya kukagua ufanyaji wa shughuli hizo na athari wanazozipata wananchi.

Alisema ili kuhakikisha usalama wa mazingira na wananchi, muongozo umetolewa kuonesha utaratibu wa kufanya shughuli hizo bila ya athari za kimazingira katika siku za baadae.

Alifahamisha kwamba uwepo wa viwanda hivyo karibu na makaazi ya wananchi kunasababisha madhara mbali mbali yakiwemo ya uharibifu wa mazingira, afya na hata vipando vyao.

Aidha waziri huyo alisema licha ya serikali kuwasisitiza wananchi kuwekeza katika shughuli za kiuchumi, hawapaswi kuachiwa kuleta athari ambazo zitavuruga mfumo mzima wa maisha yao.

Sambamba na hayo alisema zoezi hilo litakuwa endelevu kwa kuangalia viwanda vyote vinavyofanya shughuli hizo ili kuvifanya viwanda hivyo kufanya shughuli zake kwa ufanisi na kuondosha malalamiko.

Mbali na hayo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wanapobaini hitilafu yoyote juu ya uharibifu wa mazingira kwa namna moja au nyengine ni vyema kuripoti sehemu husika ili serikali iweze kufuatilia na kuchukua hatua za haraka kabla hakujatokezea athari.

Alifahamisha kwamba wapo baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakitoa huduma muhimu kwa jamii ikiwemo kuchimba visima kwa ajili ya kupatikana maji safi na salama pamoja na huduma nyenginezo.

Hata hivyo aliwasisitiza wawekezaji hao kutotumia mwanya huo kwa kuwakandamiza wengine kwani kila mtu ana haki ya kuishi ndani ya nchi kwa amani bila ya kubughudhiwa.

Hata hivyo aliwataka wawekezaji na wananchi kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayohusiana na uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kulipa umuhimu suala la uhifadhi wa mazingira.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira, Sheha Mjaja Juma, alisema ni vyema kwa viwanda vyote vya matofali hivi sasa kufuata utaratibu wa zamani wa kufanya matofali matupu kutokana na rasilimali ya mchanga hivi sasa upatikanaji wake hauna shida.

Mjaja alisema endapo wananchi hao wanataka kufanya biashara ya kusaga kokoto ni vyema mashine zao kuzihamishia maeneo ya kuchimbwa mawe ili kuondosha usumbufu na athari zinazojitokeza katika maeneo hayo.

Naye Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Nishati na Madini, Omar Saleh Mohammed, alisema hivi sasa wapo katika kufanya marekebisho kwa baadhi ya kanuni ya maliasili zisizorejesheka hivyo suala hilo likikaa sawa wataweza kutoa maelekezo yanayostahiki katika maeneo hayo.

Baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na kiwanda cha kokoto na matofali kilichopo shehia ya Mangapwani, Abdu Suleiman Juma, alisema uwepo wa kiwanda hicho kimewaathiri kiafya na kuharibika kwa vipando vyake.

Alisema katika eneo hilo yeye alilima mazao yakiwemo ya vanilla, matango na bidhaa nyengine lakini zote hakubahatika kuvuna kutokana na kuharibika na vumbi linalotoka kiwandani hapo na kusababisha kupata athari kubwa.

Kwa upande wake, Mmoja ya wamiliki wa kiwanda hicho, Soud Abdallah Nassor, alisema malalamiko hayo yapo kwa muda mrefu kutokana na Zanzibar kutotengewa maeneo maalum ya viwanda na makaazi ya wananchi.

Alieleza kuwa hali hiyo husababisha kutokezea kwa tofauti hizo na kutumia fursa hiyo kuiomba serikali kuliangalia suala hilo kwa upana wake ili kila mtu aweze kunufaika na kuishi kwa amani.

Waziri huyo alifanya ziara hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwamba viongozi waende kwa wananchi kusikiliza changamoto zinazowakabili.