NA JOHN CHACHA, PEMBA

MAKAMU wa Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Isdor Mpango, amesikitishwa na ucheleweshwaji wa ujenzi wa nyumba za askari polisi kisiwani Pemba na amemuagiza waziri wa mambo ya ndani kufika Pemba kukagua na kutathimini ujenzi wa nyumba hizo.

Kauli hiyoo ameitoa mkoa wa Kusini Pemba wakati alipofanya ziara na kukagua mradi wa nyumba za askari polisi zilizopo shehia ya Mfikwa Mkoa wa Kusini Pemba.

Dk. Mpango alisema amesikitsihwa kusuasua kwa ujenzi wa nyumba hizo na kuhoji kwanini zimechukua muda mrefu, ambapo ujenzi wa nyumba hizo 14 ulianza mwaka 2018 na mpaka sasa ni nyumba tatu zilizokamilika.

Aidha alisema kuwa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan imejipanga katika kushughulikia changamoto mbalimbali za vyombo vya ulinzi na usalama.

Alisema serikali itahakikisha inawatia vitendea kazi na vifaa vingine pamoja na maslahi yao ikiwemo makaazi na nyumba za kuishi za karibu na kambi zao, ili kuwezesha vyombo hivyo kutekeleza majukumu yake vizuri.

Makamu huyo alivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kwande wa Tanzania bara na Visiwani, kwa kuendelea kudumisha na kulinda amani iliyopo nchini na kuwaomba wananchi kuwapa ushirikiano hasa kwa kutoa taarifa za uhalifu.

Dk. Mpango, aliwataka maofisa na askari wa Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Kusini Pemba kutunza vifaa vilivyopo eneo la ujenzi kama nondo na mabati na kuwa matumizi kwa ajili ya ujenzi wa makazi na nyumba za askari zinakuwa na thamani halisi.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa huo wa Kusini Pemba, Matar Mohamed Masoud alimuomba Dk. Mpango serikali iwezeshe kujengwa kwa vituo vya Polisi katika barabara ya Ole – Kengeja ili kudhibiti uhalifu hasa wa mazao ya mifugo.

Naye Kamishna Polisi Zanzibar, Mohamedi Haji Hassan, alimueleza Dk.  Mpango kuwa ujenzi huo ulioasisiwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mhandisi Hamadi Masauni.

Alisema ujenzi umechukua muda mrefu kukamilika ambapo kunawafanya  maofisa na askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba kuishi nje na kambi zao.

Makamu wa Dk. Philip Isdor Mpango akiwa katika Mkoa wa Kaskazini Pemba amekagua ujenzi wa nyumba ya kufikia wageni wa askari Polisi ulioanza kujengwa mwaka 2016.

Kutokana na hali hiyo, alimuagiaza waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa George Simbachawene kutumia vyanzo vya ndani vya mapato vya wizara hiyo kukamilisha sehumu ya ujenzi wa nyumba hiyoo ya kufikia wageni wa askari polisi.