Aahidi mageuzi ya muundo wa tume

 Ataka mapambano yake shirikishi jamii

NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ataifanyia mabadiliko makubwa tume ya kuratibu na kudhibiti dawa za kulevya na kuwa mamlaka kamili ya kupambana na dawa hizo.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika maadhimisho ya kupinga matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil uliopo Kikwajuni.

Alisema atabadilisha muundo wa tume hiyo na kuwa mamlaka ambayo itakuwa na kikosi cha kupambana na dawa za kulevya ambapo chombo hicho kitakuwa cha kijeshi na kuwaahidi kila wanapobidi na kuhitaji msaada basi atawaongezea nguvu katika kuhakikisha janga hilo linatokomezwa.

Alifahamisha kuwa serikali itaendelea kutimiza wajibu wake katika mapambano ya kukabiliana na biashara, uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya kwa kumchukulia hatua yeyote atakayebainika kujihusisha na shughuli za dawa za kulevya.

Alisema kazi hiyo ataifanya bila ya ajizi, kuchoka na kumuonea mtu muhali hasa ikizingatiwa kuwa janga hilo linaendelea kuhatarisha vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Dk. Mwinyi alisema serikali itaimarisha vyombo vya dola vinavyoongoza mapambano dhidi ya uhalifu huo kwa kuvipatia vifaa vya kisasa vya uchunguzi na mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji sambamba na kuimarisha ulinzi katika viwanja vya ndege, bandari rasmi na bandari bubu.

Alibainisha kuwa serikali itaendelea kuzisimamia sheria na kuziongezea makali kila inapobidi pamoja na kushirikiana na jumuiya za kimataifa katika kukabiliana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya duniani.

Alisema katika madhila yanayomkosesha usingizi ni changamoto ya dawa za kulevya na udhalilishaji kwani kila asubuhi anasikia na kusisitiza kuwa sasa wakati umefika kupambana na matatizo hayo.

Alibainisha kuwa janga hilo limesababisha athari za kiafya, kiuchumi na kijamii na yanasababisha kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu kama wizi na unyang’anyi, kusababisha vifo, ajali, magonjwa ya akili na magonjwa ya kujamiiana, ulemavu na kuongezeka kwa umasikini.

Alifafanua kuwa madhara yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya yanasababisha majanga kwa wananchi na kikwazo cha maendeleo na ustawi wa jamii ya Zanzibar.

“Nimekuwa nikipokea malalamiko kwa baadhi ya wananchi kuchoshwa na changamoto zinazosababishwa na vijana wetu waliojiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya hasa kukosekana kwa amani na utulivu katika baadhi ya mitaa yetu,” alisema.

Hata hivyo, alisema serikali kupitia vyombo vya ulinzi na taasisi za sheria pekee hawawezi kufanikiwa bila ya mchango wa raia wema na wananchi kuunga mkono katika mapambano hayo.

Sambamba na hayo alibainisha kuwa taarifa zinaeleza kuwa kiasi cha watu 10,000 hasa vijana Zanzibar wanatumia dawa za kulevya kati ya hao 3,200 wanatumia dawa hizo kwa kujidunga sindano ambacho ndio chanzo kikuu cha kuenea kwa kasi maradhi ya UKIMWI homa ya ini, moyo, figo na ugonjwa wa akili.

Aliwataka wananchi na viongozi wote kutafahari iwapo wamechukua hatua muafaka za kukabiliana na janga hilo katika nchi ili kuihami na kuwaokoa vijana ambao ni tegemeo la taifa.

Alisema bado wana kazi kubwa ya kufanya katika kuiokoa jamii na balaa hilo hivyo wote kwa umoja wao kutafakari na kubuni mbinu, mipango na mikakati imara itakayoweza kutumika katika kupambana na janga hilo.

Hivyo, aliitaka ngazi ya familia katika malezi kuwafunza watoto maadili mema na kuwaelimisha athari zinazotokana na madawa ya kulevya, kutolewa elimu katika maskuli na kuwafundisha vijana stadi za maisha ili waweze kujitambua na kujilinda.

Alisema ni jukumu la viongozi wa dini na wasanii kushirikiana pamoja katika kupambana na janga hilo ili tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya Zanzibar liwe historia kwa jamii inayokuja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya kitaifa ya Uratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdullah alisema wapo katika hatua ya kupeleka mapendekezo ya kuundwa mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya.

Alisema kwenye mapendekezo hayo katika vyombo vya maamuzi hawatapendekeza watu ambao hawana sifa na badala yake kupendekeza watu maalum watakaopewa dhamana ya kusimamia jambo hilo hata mwenendo wa kesi hawatokubali kesi kukaa kwa muda mrefu bila ya kumaliza.

Hemed alisema kazi hiyo siyo ya tume pekee bali ni wazanzibari wote na kuwaomba kuunga mkono juhudi hizo za kupiga vita uingizaji na usambazaji wa dawa ndani ya nchi.

“Rais tupe ruhusa kwa hili ikiwa sheha kwenye eneo lake kuna mtu anauza dawa za kulevya halafu hatoi taarifa basi abadilishwe kwani hawezi kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya nane ilivyokusudiwa,” aliomba.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Kitaifa ya Uratibu na Udhibiti wa dawa za kulevya Luteni Kanali, Burhan Zubeir Nassor, alisema ripoti ya utafiti ya mwaka 2010 ya shirika la umoja wa mataifa la kupambana na dawa za kulevya na wahalifu duniani ilibainisha kuwa Zanzibar inakadiriwa kuwa na watu 10,000 wanaotumia dawa za kulevya.

Alisema idadi hiyo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku na kupelekea vitendo vya udhalilishaji na wizi ambapo imekuwa tishio kwa afya na ustawi wa binaadamu hasa kwa vijana, watu wazima, usalama wa taifa na utawala wa sheria.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili katika mapambano hayo alisema ni pamoja na jiografia ya upana wa kuwepo katika bahari ya hindi kwani Zanzibar imezungukwa na bahari na kubainisha kwamba Zanzibar kuna bandari bubu 371 ambazo zinatumika kwa biashara ya magendo na bidhaa mbalimbali hali inayopelekea urahisi wa walanguzi kuweza kusafirisha dawa hizo.

Changamoto nyengine ni jeshi la Polisi juu ya utendaji wao ikiwemo baadhi ya watendaji kutowajibika ipasavyo na wananchi kutokwa imani kwani mwaka 2019/ 2020 kati ya kesi 314 zilizokamatwa kesi 262 zimefungwa katika vituo vya polisi bila ya kupelekwa mahakamani.

Sambamba na hayo alibainisha kuwa changamoto nyengine inatokana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali kwani mwaka 2018/2019 kesi 70 zimefungwa mahakamani kesi 20 zimefutwa kutokana na mkemia kutofika mahakamani kutoa ushahidi.

Kwa upande wa mahakamani alisema taasisi hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi katika mapambano hayo kwa kudai kukiukwa kwa sheria ikiwemo kukosekana kwa ushahidi uliokamilika.

Alimuahidi hatomuangusha na kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa na kutokuwa na muhali na mtu yoyote ili kuhakikisha Zanzibar bila ya dawa za kulevya inawezekana.

Mwakilishi wa waliopata nafuu akitoa salam za waliopata nafuu kwa niaba ya Jumuiya ya waliopata nafuu Mikidad Kassim alisema; wanakabiliwa na changamoto hasa kwa vijana wanapopata nafuu kurudia tena hivyo ni vyema kuwezeshwa ili kuweza kupata kazi ya kufanya kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.