Asema vitapunguza uhaba mkubwa wa dawa

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaunga mkono azma ya Bohari ya Dawa (MSD) ya kutaka kujenga kiwanda hapa Zanzibar.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Meja Jenerali, Saali Mhidze akiwa amefuatana na ujumbe wake.

Alieleza kwamba azma ya MSD ya kuwekeza viwanda vya dawa hapa Zanzibar itasaidia kwa kiasi kikubwa hasa katika wakati huu wa janga la COVID 19 ambapo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka nje sio mzuri.

Alitoa pongezi kwa hatua zilizoanza kuchukuliwa na MSD za kutaka kuanzisha viwanda hapa Zanzibar ambazo zitasaidia kutatua  utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi hali ambayo athari yake inaweza  kuonekana hasa katika kipindi hichi cha maradhi ya COVID 19 duniani.

Alisema kuwa hatua hiyo ya kuanzisha viwanda inaungwa mkono na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba tayari imeshatenga maeneo maalum ya viwanda na serikali iko tayari kutoa ushirikiano wake.

Dk. Mwinyi alieleza ipo haja ya kuonekana kwamba bidhaa zinazozalishwa  Zanzibar nazo ni sehemu za biashara kutoka Tanzania  na kuondoa vikwazo vya kibiashara ambavyo hapo siku za nyuma  vilikuwepo na kusababisha biashara kati ya  sehemu mbili za muungano kuwa ngumu.

Pia, alieleza azma ya Zanzibar ya kufanya bidhaa zozote zinazozalishwa hapa nchini kuagizwa nje ya nchi huku akieleza jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyoungana na Bohari ya Dawa ya kuanzisha viwanda vya ndani hapa hapa nchini.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano mkubwa kwa Bohari ya Dawa, ili kuhakikisha azma yao hiyo inapatiwa ufumbuzi wa haraka hasa ikitambua kwamba ina uwezo na uzoefu mkubwa katika fani hiyo.

Rais Dk. Mwinyi aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuwa na viwanda vya aina mbali mbali lakini soko lake ni dogo ikilinganishwa na soko la Tanzania Bara na soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kueleza haja kwa Bohari ya Dawa kueleza taratibu zinazohitajika ili kuondoa usumbufu kwa bidhaa zinazotoka Zanzibar.

Alisema  kuwa ni vyema Bohari ya Dawa MSD, ikatoa maelekezo mazuri ili  kuepuka kufanyika uzalishaji  wa bidhaa kutoka Zanzibar na baadae kupata usumbufu wa soko la nje ya Zanzibar.

Aidha, Dk. Mwinyi ameeleza haja ya MSD kuleta vijana ili kutoa utaalamu na mafunzo kwa watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujifunza  juu ya mfumo wa ununuzi, uhifadhi, usambazaji dawa, vifaa na vifaa tiba.

Alisema kwamba iwapo Zanzibar itapata utaalamu kutoka MSD mafanikio zaidi yatapatikana katika mfumo mzima wa utoaji wa huduma hiyo hasa ikizingatiwa kwamba utaalamu huo kwa Zanzibar haujawa wa kuridhisha zaidi.

Awali Meja Jenerali Saali Mhidze akitoa maelezo alisema kuwa MSD, inadhamiria kuja kuwekeza Zanzibar kiwanda cha dawa ambacho kitakuwa kikubwa kwa Tanzania, ukanda wa Afrika Mashariki na hata nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Alisema kuwa dhamira ya MSD ya kuja kujenga kiwanda cha dawa hapa Zanzibar inatokana na mahitaji ya dawa na vifaa tiba vyenginevyo hapa nchini hasa katika wakati kama huu wa uwepo wa maradhi ya COVID 19 ambapo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi ni mgumu.

Alieleza MSD, inachukua hatua za makusudi za kuhakikisha inajenga viwanda kwa ajili ya utoaji wa vifaa hivyo na tayari kwa upande wa Tanzania Bara wameshaanza ujenzi wa viwanda kama hivyo.

Alisema MSD imekusudia kupanua upatikanaji wa dawa na vifaa tiba hapa nchini na tayari viwanda vinne vimeshakamilika kazi tangu mwezi Oktoba mwaka uliopita na kwamba baada ya miezi mitatu uhaba wa dawa unaweza kupungua.

Meja Jenerali Mhidze alisisitiza kwamba hatua za ujenzi wa kiwanda  cha dawa hapa Zanzibar pia, kutasaidia kuleta ushirikiano wa uzalishaji wa dawa katika viwanda kati ya vile watakavyojenga Tanzania Bara na vile vya Zanzibar.

Sambamba na hayo, Meja Jenerali Mhidze alimuhakikishia Dk. Mwinyi kwamba kufanikiwa kwa azma yao hiyo ya ujenzi wa kiwanda cha dawa hapa Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa dawa hapa hapa nchini.