NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza serikali ya Ujerumani kwa utayari wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Regine Hess.
Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Hess kuwa azma ya serikali ya Ujerumani ya kuendelea kuisaida Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuyafikia malengo yaliyowekwa.
Alisema kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia, inathamini sana mashirikiano yaliyopo kati yake na serikali ya Ujerumani na hatua yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya afya ambayo itaendelea kuiletea manufaa makubwa kwa wananchi wa Zanzibar.
Alisema azma ya serikali ya Ujerumani ya kusaidia uendelezaji wa mradi wa maji safi na salama na mitaro ya maji taka katika eneo la Mji Mkongwe itasaidia katika kuuweka vizuri mji huo.
Alifahamisha kuwa serikali ya Ujerumani kwa muda mrefu imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya afya hapa nchini ikiwa pamoja na kuzisaidia hospitali ya Abdalla Mzee Pemba na Hospitali ya Kijeshi ya Bububu.
Hivyo, Dk. Mwinyi alieleza kwamba mbali ya Zanzibar kusaidiwa katika kuendeleza miradi katika sekta ya afya ni vyema ikasaidiwa katika uendelezaji miundombinu na mifumo ya afya pamoja na uendelezaji wa rasilimali watu ili kuwe na tija endelevu ya misaada inayotolewa.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Ujerumaini kuja kuwekeza Zanzibar kwa kutumia fursa zilizopo hasa kupitia sera yake ya uchumi wa buluu kwani ndani yake mna mambo mengi ya kuwekeza yakiwemo utalii, uvuvi, mafuta na gesi pamoja na kuzitumia rasilimali nyengine za bahari.
Katika suala uwekezaji, Dk. Mwinyi alisema kuwa serikali, tayari imeshaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na iko tayari kuwapokea.
Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Serikali ya Ujerumaini kuiunga mkono Zanzibar katika mapambano dhidi ya maradhi ya COVID 19 ambayo yameikumba dunia nzima.
Mapema, Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess, kwa upande wake alisema kuwa Zanzibar na Ujerumani zina historia kubwa ya mashirikiano hivyo Ujerumani itayaendeleza mashirikiano hayo kwa kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Nane katika kuendeleza miradi iliyojiwekea.
Balozi Hess alimueleza Dk. Mwinyi kwamba Serikali yake iko tayari kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo huduma za maji safi na salama pamoja na mitaro ya maji taka katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Aliongeza kuwa Mji Mkongwe wa Zanzibar una mashirikiano mazuri na Serikali ya Ujerumani kwani miradi kadhaa ya miundombinu yake imetekelezwa na nchi hiyo.
Aidha, Balozi Hess alisema kuwa kwa upande wa Sekta ya afya Serikali ya Ujerumari iko tayari kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo hapa nchini.
Balozi Hess pia, alimuhakikishia Dk. Mwinyi kwamba juhudi za makusudi zitachukuliwa na Ubalozi huo katika kuitangaza Zanzibar kiutalii ikiwa ni pamoja na kuwaleta wawekezaji kutoka Ujerumani kuja kuwekeza hapa Zanzibar.