Asema kuna fursa kudekede

NA TATU MAKAME

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinzduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali imejipanga kuzitumia fursa za bahari ikiwemo kutekeleza uvuvi wa kisasa utakaosaidia ukuaji wa uchumi na kuongeza pato la taifa.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo jana huko katika hoteli ya Verde iliyopo Mtoni, wakati akifungua kongamano la uchumi wa buluu kwa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.

Alisema katika kufanikisha utekelezaji wa uvuvi wa kisasa kama mojawapo ya mipango ya uchumi wa buluu, serikali imepanga kununua zana za kisasa za uvuvi ambazo zitasaidia uvunaji wa raslimali zilizomo baharini huku kukizingatiwa uhifadhi wa mazingira.

Alifahamisha kwamba sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta muhimu kwa uchumi hasa ukizingatia kuwa Zanzibar imebarikiwa kuwa na raslimali hizo, hivyo zinapaswa kutumika kwa mujibu wa mipango na kukuza soko la bidhaa hizo ikiwemo usarifu wa samaki na kutengeneza ajira zaidi kwa wananchi wake.

Dk. Mwinyi alifahamisha kuwa ili kuona dhana ya bahari inatumika vyema na kuwa endelevu ni vyema kuendelea kuwapatia wananchi elimu juu ya kuendeleza harakati za uvuvi sambamba na kuwahamasisha juu ya uanzishwaji wa viwanda na masoko.

Akizungumzia uwekezaji katika sekta hiyo, Dk. Mwinyi alisema serikali inaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa kampuni za utafiti na gesi asilia na wenye nia njema ya kuwekeza na kuinua uchumi wa Zanzibar pamoja na kuharakisha ujenzi wa bandari ya Mangapwani.

Alisema kongamano hilo ni sehemu ya jukwaa la maendeleo endelevu linalofanywa na taasisi ya uongozi kila mwaka, hivyo kufanyika visiwani Zanzibar kutaongeza nafasi kwa wananchi wanaoendelea kutumia bahari kwa manufaa yao.

Hata hivyo, Dk. Mwinyi alisema lengo la kongamano hilo ni kuhamasisha maendeleo jumuishi na endelevu yanayozingatia utunzaji wa mazingira na matumizi bora ya rasilimali kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vya baadae.

“Kama ambavyo nilikuwa nikinukuliwa kwenye hotuba zangu zilizopita, serikali ya awamu ya nane ina dhamira ya dhati ya kupanua wigo wa matumizi endelevu ya bahari na raslimali zetu ili kujenga uchumi imara kwa taifa letu”, alisema

Dk. Mwinyi alisema bado kuna fursa na faida za uwekezaji zaidi chini ya uchumi wa buluu kama ukulima wa mwani na ujenzi wa miundombinu ya kimkakati ya usafiri baharini zikiwemo utalii wa fukwe na michezo.

Kwa upande wake waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Abdalla Hussein Kombo alisema wizara hiyo itaendelea kuimarisha mazingira bora katika kuhakikisha dhana ya uchumi inafikia malengo.

Mapema akiwasilisha mada mtafiti mwandamizi, taasisi ya uongozi, Prof.  Joseph Semboja alisema ipo haja kwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuongeza jitihada za kuendeleza uchumi wa buluu ili kuingia kwenye uchumi shindani na mataifa mengine duniani.

Kongamano hilo la siku moja lilijadili njia bora zitakazosaidia matumizi bora ya bahari kwa kuzingatia mazingira, ambapo limeandaliwa na taasisi ya uongozi, Shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Shirika  la Umoja wa Mataifa la Uhifadhi wa Mazingira la (UNEP) likiwa na kauli mbiu  ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi, na uhifadhi wa mazingira.