NA ABOUD MAHMOUD

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmin katika kilele cha maadhimisho wa wiki ya Utumishi wa Umma Juni 23 mwaka huu.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman huko Ofisini kwake Mazizini, alisema kilele cha maadhimisho hayo inatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni mjini Unguja.

Waziri Haroun, alisema kupitia maadhimisho hayo Zanzibar inaungana na nchi nyengine barani Afrika na duniani kote kuthamini mchango wa utumishi wa umma katika maendeleo ya jamii.

“Kama inavyofahamika maadhimisho ya wiki ua utumishi wa umma hapa Zanzibar yalianza mwaka 2019 ambapo mgeni rasmin alikua Dk. Shein Rais wa awamu ya saba na mwaka 2020 kutokana na janga na coroana hayakufanyika  na mwaka huu tumeamua kuendelea na maadhimisho hayo,”alisema.

Aidha Waziri huyo alieleza kuwa ofisi yake imejipanga katika siku zijazo kuongeza upeo wa utekelezaji wa maadhimisho hayo kwa kuongeza mashirikiano ya Wizara na taasisi zote za umma ili tija Zaidi iweze kupatikana.

Katika maadhimisho hayo kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma ni kichocheo cha kuimarisha utoaji wa huduma katika jamii’.

Waziri Haroun alisema ujumbe huo unalenga kuleta mabadiliko chanya na yenye tija kwa watumishi wa umma, jamii na taifa kwa ujumla.

Alifahamisha kuwa hii inatokana na sababu ya uwajibikaji na uadilifu imekua ndio kilio kikubwa anachokisisitiza mara kwa mara Dk. Mwinyi.

“Kwa kutumia ujumbe huu watumishi wa umma tunatakiwa tubadilike kiutendaji ili kuleta katika kazi zetu,”alifafanua.

Sambamba na hayo Waziri Haroun alitoa wito kwa wananchi kuendelea kumuunga mkono Dk. Mwinyi katika jitihada zake za kuwajibika vyema na kufanya uadilifu kwa dhamana walizopewa.