Wasisitiza ushirikiano katika muungano

Wapongeza kasi utatuzi changamoto mazingira

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amekutana na kuzungumza na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philp Esdori Mpango, ambapo viongozi hao  walisisitiza kuendeleza mashirikiano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Viongozi hao walifanya mazungumzo hayo jana katika ukumbi wa ikulu jijini Zanzibar ambapo mazungumzo hayo pia, yalihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano na viongozi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Mwinyi alimueleza Dk. Mpango kuwa anafarajika na juhudi zinazoendelea za mashirikiano yaliyopo ya Muungano ambapo zinazidisha ushirikiano uliopo kuimarika.

Alieleza kuwa kutokana na mashirikiano hayo  yamesababisha changamoto zilizopo kushughulikiwa kwa haraka  kwa azma ya kuijenga nchi katika pande zote  za Muungano.

Akieleza kuhusu suala zima la mazingira, Dk. Mwinyi, alisema licha ya kuwa suala la mazingira si la Muungano, lakini lina umuhimu wa kushughulikiwa kwa pamoja kwa pande zote mbili.

Alieleza kuwa uharibifu wa mazingira si jambo la kubezwa hasa katika visiwa vya Unguja na Pemba, hivyo kuna kila sababu ya kuimarisha ushirikiano katika jambo hilo.

Aliongeza kuwa kumekuwepo na mashirikiano mazuri kati ya pande mbili hizo hata katika mambo yasiyohusiana na Muungano ambapo hata kwa upande  wa wizara za Zanzibar zimepata fursa ya kujifunza mambo kadhaa kutoka katika upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano.

Naye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, alitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kwa mapokezi mazuri.

Dk. Mpango alieleza dhamira ya kuifanya Zanzibar kuwa ni sehemu yake ya mwanzo ya kufanya ziara rasmi tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo na kueleza jinsi alivyofarajika na mwanzo huo mzuri aliouanza.

Aidha, Makamu wa Rais huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alieleza malengo ya ziara yake fupi ya kuja kumsalimu Rais pamoja na wananchi wa Zanzibar ambapo pia, atapata fursa ya kukutana na watendaji katika taasisi ambazo zinashughulikia masuala ya Muungano.

Alieleza jinsi alivyofurahishwa na hatua  za Dk. Mwinyi katika kukuza uchumi hasa katika kipindi cha uwepo wa maradhi ya COVID 19, ambapo bado uchumi wa nchi uko vizuri, wastani wa mfumko wa bei ni mdogo na kuendeleza vizuri kwa kipato cha wananchi.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Mwinyi kwa kuendeleza kasi ya uchumi na kutekeleza azma yake ya kusimamia uchumi ambapo maisha ya wananchi yamekuwa yakitegemea nguvu za uchumi huo na kueleza kwamba hatua hizo zinatokana na ile azma yake ya kusimamia Mapinduzi ya Uchumi hapa Zanzibar.

Aliongeza kuwa hatua za Dk. Mwinyi za kujikita katika uchumi wa buluu ambao unahusisha rasilimali za bahari, uvuvi, ufugaji wa samaki, miundombinu ya bandari, utalii na sekta nyenginezo, zinaonesha imani yake kubwa aliyonayo katika kuiletea maendeleo endelevu Zanzibar.

Dk. Mpango alipongeza hatua za Dk. Mwinyi katika suala zima la utawala bora ambao ndio msingi wa maendeleo ambapo amekuwa akipambana na suala zima la rushwa, ufisadi,uzembe kazini sambamba na kuweza kuchukua hatua.

Alisisitiza kwamba Rais Dk. Mwinyi ameweza kufanikiwa katika kuhakikisha matumizi ya fedha za Serikali yanakwenda vizuri na kueleza kwa upande wao wameweza kujifunza juhudi zake hizo.

Dk. Mpango alitoa pongezi kwa Dk. Mwinyi kwa jinsi anavyoendeleza vizuri ushirikiano wa Kimataifa ambapo washirika wa maendeleo wameendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Alisema kuwa juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuimarisha Muungano na kueleza haja ya kuendelea kuzishughulikia changamoto za Muungano ambapo tayari changamoto kadhaa zimeshapatiwa ufumbuzi.