NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuna kazi kubwa inayohitaji kufanywa ili kuwa na wataalamu wa kutosha hasa katika utoaji wa huduma za upasuaji.

Dk. Mwinyi alisema hayo jana huko katika ukumbi wa hoteli ya Madinat Al Bahr Mbweni, nje kidogo ya jiji la Zanzibar wakati akiufungua mkutano mkuu wa madaktari wa upasuaji Tanzania (TSA).

Dk. Mwinyi alieleza kuwa mara nyingi wagonjwa wanaohitaji huduma za upasuaji hulazimika kupatiwa rufaa nje ya nchi, jambo ambalo lina gharama kubwa kwa serikali na lenye kuleta usumbufu kwa wagonjwa na wanafamilia wanaouguliwa.

Aliongeza kuwa ikiwezekana kuwa na wataalamu wa kutosha wa upasuaji kwa maradhi mbali mbali yanayowasibu wananchi itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji katika sekta ya afya ambazo hadi sasa ni kubwa.

Alisema serikali zote mbili zinahitaji kuwa na mikakati imara ya kupunguza upelekaji wa wagonjwa nje ya nchi ili kupunguza gharama ambapo alitolea mfano kwa upande wa Zanzibar katika kipindi cha Julai mwaka 2019/2020, jumla ya wagonjwa 726 walipatiwa rufaa nje ya Zanzibar na matibabu yao yaligharimu shilingi bilioni nane.

Aidha, alisema kuwa kwa mwaka uliofuata Julai 2020 hadi Juni 2021, jumla ya wagonjwa 239 walipatiwa rufaa nje ya Zanzibar na matibabu yao yaliigharimu serikali shilingi bilioni 3.7 idadi ya wagonjwa kwa mwaka huo imeshuka kutokana na kuzuia wagonjwa kusafiri nje ya nchi kwa sababu ya mripuko wa ugonjwa wa Korona.

Sambamba na hayo, Dk. Mwinyi alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana bado sekta ya afya imekabiliwa na changamoto nyingi katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kuwa ushauri wao unahitajika juu ya namna bora ya kuimarisha miundombinu na mifumo ya afya ili kuweza kwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia na kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo nchini.

Dk. Mwinyi alieleza kwamba serikali zote mbili bado zinahitaji ushauri wa wataalamu hao katika kutatua rasilimali fedha, vifaa na nyenzo mbali mbali zitakazoendesha huduma za afya  kwa ufanisi zaidi.

Aliongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar wanaweza kushauri juu ya namna bora ya kutekeleza dhamira ya kuanzisha bima ya afya, ambayo itasaidia kuimarisha huduma na upatikanaji wa rasilimali fedha zinahitajika, wakati huo huo, Serikali inaendelea kutoa huduma kwa wananchi wasio na uwezo wa kukata bima hiyo.

Kadhalika, alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho janga la maradhi ya COVID 19 linaendelea kutikisa dunia, wao wataalamu wana jukumu kubwa la kuzishauri Serikali juu ya njia bora ya kukabiliana na maradhi hayo.

Alisema kuwa ndio maana hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameunda timu ya wataalamu ili kushauri juu ya njia bora ya kukabiliana na maradhi ya COVID-19.

Hivyo, aliwataka wataalamu hao kuendelea kushirikiana na Serikali na kuzishauri vizuri ili zipate mafanikio makubwa zaidi.

Dk. Mwinyi aliwahimiza madaktari hao kuendelea kujifunza mambo mapya na katu wasitosheke na ujuzi na utaalamu walionao kwani imani yake ni kwamba wana uwezo mkubwa wa kutoa huduma na kuvutia watu kutoka mataifa mbali mbali kuja kufuata huduma za upasuaji na tiba nyengine hapa Tanzania.

Aliwataka madaktari hao nao kwa upande wao kutumia fursa hiyo kuja Zanzibar kutoa huduma za upasuaji ili kuisaidia Serikali kupunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.

Mapema  Rais wa Madaktari wa Upasuaji Tanzania (TSA), Dk. Catherine Mng’ongoro alieleza jinsi hatua mbali mbali zinazochukuliwa na (TSA) katika kuendeleza na kuimarisha huduma za upasuaji.

Kiongozi huyo alitoa shukurani kwa Wizara ya Afya kwa kutoa ushirikiano mkubwa wa kufanikisha mkutano huo hapa Zanzibar.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dk. Marijani Msafiri alisema kuwa hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja imekuwa ikifanya shughuli nyingi mbali ya kutoa tiba pia, imekuwa ikifundisha, kufanywa tafiti na shughuli nyeginezo.

Alisema kuwa tayari madaktari bingwa 42 wa fani mbali mbali wapo Zanzibar na wauguzi bingwa wapatao 24 hasa katika huduma za dharura, mama na mtoto na wagonjwa mahututi ambapo pia huduma za upasuaji wa uti wa mgongo na ubongo, saratani,upasuaji wa watoto, matibabu ya mfumo wa njia ya chakula, uchunguzi wa maradhi ya vichocheo vya mwili, matibabu ya ngozi, pua, koo masikio na mengineyo.

Dk. Marijani alieleza mafanikio yaliyopatikana katika huduma za maabara ikiwa ni pamoja na kuwasomesha madaktari bingwa katika fani hiyo huku akieleza viwango vya ubora ilivyopata Hospitali Kuu ya MnaziMmoja.