Ataka wazidishe uwajibikaji, ubunifu
NA KHAMISUU ABDALLAH
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka watumishi wa umma wa Zanzibar kuwa waadilifu na kutojihusisha na vitendo vya ukiukaji wa maadili ili kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi na watu wake.
Alisema hali hiyo inatokana na mchango mkubwa walionao katika mabadiliko yatakayoinua hali ya uchumi wa nchi na kufikia kiwango cha juu cha uchumi wa kati kama ilivyoelekekezwa katika dira ya maendeleo ya Zanzibar 2050.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana katika kilele cha maadhimisho wiki ya utumishi wa umma yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni mjini Zanzibar.
Alisema watumishi wa umma wana dhamana wa kuishauri serikali katika utungaji wa sera na sheria, kusimamia utekelezaji wa sheria hizo pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo elimu, afya, maji safi na salama na huduma nyenginezo za jamii.
Hivyo aliwataka kutumia maadhimisho hayo kutafakari na kutathmini ufanisi na changamoto zilizomo katika utumishi wa umma Zanzibar ili kukidhi dhamira yake ya kuwania utumishi wa wananchi katika nafasi ya Urais.
Aidha Dk. Mwinyi aliwahimiza kuongeza bidiii katika kazi ili kuleta tija na ufanisi wanapotekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi na kubainisha changamoto zinazowakabili na kutafuta mbinu muafaka za kutatua changamoto hizo.
Alibainisha kuwa wameanza kuona mafanikio ya ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya serikali, ukuaji wa uchumi, kuimarika kwa nidhamu ya matumizi ya fedha za serikali na uwajibikaji.
Akizungumzia kauli mbiu ya wiki hiyo inayohimiza Uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma kama kichocheo cha kuimarisha utoaji wa huduma katika jamii, alisema inasisitiza mambo ya msingi katika utumishi hivyo ipo haja ya kila mtumishi kuizingatia.
Alisema ili kuhimiza uwajibikaji na kupiga vita vitendo vya ukiukwaji wa maadili, amekuwa akichukua hatua na kufanya mabadiliko ya watendaji kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi katika taasisi mbalimbali.
Aidha alisema hatua hizo licha ya kulalamikiwa na baadhi ya watu, zinaungwa mkono na wananchi walio wengi kwani zinafanywa kwa nia njema na sio kumkomoa mtu yoyote.
Aidha alisema taarifa iliyowasilishwa kwake na Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inatoa taswira isiyopendeza ya kukosekana kwa uadilifu na uwajibikaji kwenye baadhi ya taasisi na watumishi mbalimbali wa umma nchini.
Alisema, taarifa hiyo ilibainisha matumizi mabaya ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo, utekelezaji wa miradi chini ya viwango, wizi wa fedha za umma na ubadhilifu, baadhi ya taasisi ofisi ya mkaguzi mkuu haikupewa ushirikiano kuweza kutimiza majukumu yake jambo ambalo halikubaliki.
Vilevile Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa viongozi na watendaji wa taasisi kusikiliza changmoto zinazowakabili wananchi pamoja na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi, huku akiwataka kuepuka urasimu usio na lazima katika utoaji wa huduma.
Alisema tayari kuna mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika matumizi ya mfumo wa ‘Sema na Rais’ (SNR), na kubainisha kuwepo changamoto kadhaa zilizokwisha kupatiwa ufumbuzi.
Alitoa rai kwa wananchi kutoa taarifa zilizokamilika pamoja na kushirikiana na viongozi wanaohusika ili taarifa hizo ziweze kufuatiliwa vizuri na kufikia malengo ya kuanzishwa kwa mfumo huo.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa viongozi kujiongeza na kuleta ubunifu katika taasisi zao, akibainisha baadhi yao kutokuwa na mipango wala mikakati ya maendeleo kisekta katika taasisi wanazoziongoza na kusubiri Ofisi yake (Ikulu) iwapangie mipango hiyo.
Naye, Waziri wa Nchi, (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman aliwataka watumishi kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika taasisi na maeneo yao ya kazi.
Haroun alitumia fursa hiyo kumkabidhi tuzo maalum ya heshima Dk. Mwinyi, ikiwa ni hatua ya kuthamini mchango wake katika kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma na utawa bora nchini.
Mapema, Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Seif Shaaban Mwinyi, alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo inalenga kuwahamasisha watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akiwasilisha mada ya ‘Hali ya Utumishi wa Umma Zanzibar na hatua zilizochukuliwa katika kuimarisha uwajibikaji’, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi, (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mansura Mossi Kassim, alisema miongoni mwa changamoto ziliopo ni ya kutokuwepo kwa chombo rasmi kinachoratibu mafunzo ya utumishi wa umma, huku kila taasisi ikifanya shughuli hiyo pekee.