Ataka fursa ya uwekezaji isikwamishe malipo

Ateua bosi mpya shirika la nyumba

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameutaka uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kutambua kwamba madhumuni ya mfuko huo ni kuwasadia wastaafu ili waweze kuishi vizuri baada ya ustaafu wao.

 Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo , Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ukiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa mfuko huo Nassor Shaaban Ameir.

Alisema kwamba kuna utofauti mkubwa wa wastaafu wa hapa nchini na nchi nyengine duniani ambapo kwa upande wa nchi hizo wastaafu baada ya kustaafu kazi ndipo huishi vizuri zaidi kuliko wakiwa kazini.

Dk. Mwinyi, alisema kuwa watu wamekuwa wakitoa fedha zao na kuziweka katika Mfuko wa ZSSF katika kipindi  chao chote cha kazi ambapo fedha hizo zimekuwa zikiekezwa kwa miaka mingi hivyo, wamekuwa na matarajio makubwa kwamba watapata faida kubwa baada ya kustaafu lakini kinachotoka ni tofauti.

Alisema kwamba moja ya dhamana kubwa iliyopewa ZSSF ni kuhakikisha unawekeza vizuri na unatapa faida nzuri ili kuhakikisha wastaafu wanaishi vizuri na sio kupigiwa hesabu kwa walichochangia wakati wako kazini.

Dk. Mwinyi alieleza kwamba mstaafu wakati yuko kazini amekuwa akichangia hadi anafika muda wa kustaafu wa miaka 60 anakuwa ameshatengeneza faida na kueleza kwamba hakuna sababu ya mstaafu kutopata maslahi mazuri.

“Yote fanyeni lakini kinachotakiwa mwisho wa siku ni kuhakikisha watu waliochangia fedha zao wakistaafu wanalipwa vizuri”, alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba  ni vyema Mfuko huo ukawa na dhamana ya fedha za watu kwa kuekezwa vizuri ili ziweze kupata faida ya miaka yote ya wastaafu waliyoweka fedha zao.

Dk. Mwinyi alisema  kuwa  moja ya njia ya kuwasaidia wasfatu ni kuwapatia makaazi kwani wafanyakazi wa Zanzibar hawana mategemeo ya kupata makaazi mazuri kwa sababu hawana uwezo, hivyo ilikuwa  ni wajibu wa mfuko huo kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya wateja wao wa Mfuko huo ambao ni wanyonge.

Aliongeza kuwa mafao yanayotokana na ZSSF bado hayajawafurahisha wawekaji na kusisitiza kwamba Mfuko huo ni vyema ukaliangalia suala hilo hasa ikizingatiwa kwamba watu wanawekeza fedha zao katika Mfuko huo ili waje kupata faida.

Dk. Mwinyi alisema kuwa utaratibu wa Kikokotoa isiwe sababu ya kutowalipa  wastaafu kima cha fedha kinachostahiki na kueleza kuwa wastaafu ni lazima walipwe vizuri kwani ndio lengo la Mfuko huo kwani wengine wameanza kuweka fedha zao tokea wanaajiriwa wakitokea skuli hadi kustaafu kwao wakiwa na miaka 60.

Dk. Mwinyi  aliutaka uongozi wa Mfuko huo kuwa makini zaidi katika suala zima la uwekezaji wanaoufanya kwa kuhakikisha kwamba miradi wanayowekeza inakuwa na faida kwa Mfuko huo na kuangalia haja ya kusimamia vyema uanzishwaji wa Mfuko wa Bima ya Afya.

Mapema viongozi hao walieleza kwamba lengo la ZSSF ni kuwahifadhi wanachama wake wanapopatwa na majanga ambayo husitisha au kupunguza kipato kutokana na sababu mbali mbali kama vile uzee, ulemavu, maradhi, kifo, uzazi, pamoja na majanga mengineyo yanayoidhinishwa na Bodi ya Wadhamini wa Mfuko huo.

Aidha, uongozi huo ulieleza azma ya kukusanya fedha kwa  njia za elektroniki katika viwanja vyake vya kufurahishia watoto Unguja na Pemba ili kuweza kukusanya vyema mapato yake.

Uongozi huo ulieleza kwamba pamoja na kazi za kawaida ambazo Mfuko unatekeleza, pia, unaendelea kufuatilia kwa karibu maagizo mbali mbali anayoyatoa Rais ambayo yanagusa shughuli za uendeshaji wa Mfuko.

Pia, uongozi huo ulieleza azma ya kuangalia uwezekano wa kuanzisha Mafao mapya kama vile mafao ya matibabu na kadhalika sambamba na kuanzisha ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika maeneo tofauti kwa kushirikiana na Serikali kulingana na upatikanaji wa ardhi.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amemteua Mwanaisha Alli Said kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Zanzibar.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said, ilieleza kuwa uteuzi huo umeanza Juni 1, mwaka huu.