YAOUNDE, Cameroun
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Veron Mosengo-Omba, amesema, kucheleweshwa kwa droo ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyopangwa mwaka ujao itafanyika Yaounde ndani ya siku 15 za kwanza za Agosti.

Mosengo-Omba, ambaye amekuwa akisimamia timu ya ukaguzi ya CAF nchini Cameroun, alitangaza tarehe hiyo mpya wakati wa mkutano na waandishi wa habari juzi. Droo hiyo ilikuwa imepangwa kufanyika Juni 25, lakini, CAF iliahirisha.

Ripoti za mitandao ya kijamii zilionesha kuwa baraza hilo linalosimamia mpira wa miguu barani Afrika lilipanga kuondoa haki za uenyeji wa mashindano hayo kutoka Cameroun baada droo kuahirishwa. Algeria, Morocco na Misri zimetajwa kuwa mbadala zaidi.
Lakini Mosengo-Omba alihakikishia kuwa hakuna mipango ya kuchukua mashindano hayo kutoka nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

“AFCON itaandaliwa hapa nchini (Cameroun) mnamo Januari mwakani”, Mosengo-Omba, alisema katika kukanusha ripoti hizo. “Vyombo vya habari vya kijamii sio CAF … Lazima tushirikiane kutoa AFCON ambayo itakuwa ya kwanza ya aina yake barani”.

Ofisa huyo wa CAF alionyesha kufurahishwa na kiwango cha utayarishaji wa mashindano hayo akisema ni tofauti kabisa na kile amekuwa akisoma.

“Ubora wa miundombinu ni mzuri . Hiyo (Cameroun) mna viwanja vya hali ya juu. Nilitembelea uwanja wa Olembe, ni wa kiwango cha ulimwengu na inaweza hata kuandaa michezo ya Kombe la Dunia”, alibainisha, Mosengo-Omba.