NA MADINA ISSA

ZAIDI ya Euro milioni tisa zimetengwa kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo ya sekta binafsi ikiwemo kuengeza ajira katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula na lishe.

Akizungumzia fedha hizo, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo, Dk. Soud Nahoda Hassan, baada ya kikao cha majadiliano na balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya alipofika Ofisini kwake kwa mazungumzo.

Alisema, Wizara hiyo ipo tayari kutoa ajira kwa wananchi kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya, ili kuhakikisha wanafaidia na mradi huo kwani wengi watajiajiri kupata mahitaji yao kama mradi ulivyoelekeza.

Waziri huyo alisema wawekezaji wanaoingia nchini kuwekeza wanatekeleza lengo la serikali na Wizara hiyo itahakikisha  wanashirikiana nao ili kuona maisha ya wananchi yanakuwa yenye tija na mazao yao yanakuwa na kilimo bora pamoja na kukua kwa masoko.

“Kwenye kilimo hichi tutaweza kuwashauri wakulima kulima kilimo kilichokuwa bora na kuwasaidia wananchi katika rasilimali katika kukuza huduma ambao mradi huo utakuwa ni mmoja wa miradi mikubwa” alisema.

Nae, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Manfredo Fanti, alisema lengo la mradi huo ni kuboresha kilimo kwa wakulima wadogo wadogo na kuwapatia elimu pamoja na kuwasaidia wanawake kupata rasilimali na kukuza soko.