Ni binti mwenye uoni hafifu mwenye shahada ya uhasibu

NA HAJI NASSOR, PEMBA   

 “NILIZALIWA nikiwa sioni kabisa, lakini miaka mitatu baadae nilifanyiwa operesheni, nikiwa na uoni hafifu hadi nikamaliza dara sa 12,’’ndio maneno ya mwanzo ya Faiza Said Kassim.

Mwaka 2019 Faiza alikuwa mmoja kati ya wahitimu wa elimu ya digrii kwa fani ya uhasibu, kwenye Chuo cha Usimamizi wa Fedha Chwaka Zanzibar.

Mama wa Faiza, Bi Habiba Yussufu Alawi anasema kati ya mimba zake tano, ya Faiza ndio ambayo ilimtia mashaka na kulazimika kuhudhuria hospitali kila muda.

Baada ya kumzaa, aligundua hana uoni kamili, ingawa mwaka mmoja na nusu badaae, alimikimbiza hospitali kwa uchunguzi na alipotimiza miaka mitatu alifanyiwa upasuaji.

“Faiza alifanyiwa operesheni hospitali ya Muhimbili, na baada ya kukua na kuanza elimu ya msingi alianza kutumia miwani maalum,’’anasema.

Mwenyewe anasema, alikuwa na uoni hafifu tokea kupata kwake fahamu, na alianza darasa la kwanza skuli ya msingi ya Michakaini Chake chake akiwa kwenye elimu mjumuisho.

“Ijapokuwa sio lile darasa rasmi, lakini na mimi nilichanganywa na wengine wenye uoni kamili, na kuanzia hapo ikawa mimi na miwani ni ndugu,’’anasimulia.

Aliendelea na msomo yake ya msingi skulini hapo, akijinasibu kuwa tokea elimu yake msingi hadi anamaliza digrii yake ya uhasibu mwaka 2019, hakuwahi kufeli wala kurejea mitihani.

“Mimi ilikuwa nafasi yangu ya darasani kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la 12, ni kati ya tatu hadi tano, na hata nilipokuwa chuo sikuwahi kupata mitihani ya marejeo,’’anaeleza.

Akiwa skuli ya msingi ya Michakaini, anasema alikuwa na ushirikiano mzuri na wanafunzi wenzake, na wala hakuwahi kubaguliwa kwa sababu ya uoni wake hafifu, wala miwani aliyokuwa akiivaa.