NA ABOUD MAHMOUD

MAMIA ya wananchi wa Zanzibar pamoja na wasanii wa fani mbali mbali wameungana katika maziko ya mtunzi mahiri wa vitabu,mashairi na nyimbo nchini marehemu Haji Gora Haji.

Marehemu Haji Gora alifariki dunia juzi baada ya kuugua kwa muda mrefu na kuzikwa kijijini kwao Tumbatu Gomani .

Baadhi ya wasanii waliopata kuzungumza na gazeti hili  walimuelezea marehemu kuwa ni mtu mweledi ambae ameweza kuitangaza nchi kitaifa na kimataifa.

Walisema kifo cha marehemu Gora ni pigo kubwa kwa Zanzibar na Tanzania kwa  ujumla, kwani fani alizokua nazo zimesaidia kutoa elimu wa watu wa rika tofauti.

“Marehemu Mzee Gora nimemfahamu kwa kipindi kirefu kutokana na kusikiliza mashairi na kusoma vitabu alivyokua akitunga, lakini mara baada na mimi kuingia katika fani ya utunzi wa vitabu nilikua nikimtumia sana kwa ajili ya kunipa muongozo na maarifa,”alisema Amir Ali.

Amir ambae pia ni mtunzi wa vitabu alisema kwamba kifo cha Gora ni cha taifa kwani kazi zake alizozifanya zimeweza kutumika na kila mwananchi.

Ahmed Juma Mohammed msanii wa muziki wa taarab katika kundi la Nadi Ikhwan Safaa alisema katika kikundi chake marehemu watamkumbuka kutokana na yeye ni miongoni mwa watu waliosaidia kukitangaza na kukipatia umaarufu kutokana na kukitungia nyimbo mbali mbali.

Ahmed alisem Nadi Ikhwan Safaa pamoja na vikundi mbali mbali vya muziki wa taarab nchini, vimepoteza mtu muhimu ambae alisaidia fani hiyo kufika mbali na kupata umaarufu.

“Hatuwezi kusema mengi hii ni haki ya kila mmoja wetu lazima imfikie yeye ametangulia na sisi tupo nyuma yake muhimu ni kumuombea Mwenyezi Mungu amsamehe makossa yake,lakini kwetu ni mtu muhimu sana na kifo chake kimetugusa wasanii sote Zanzibar,”alisema Ahmed Juma.

Kwa upande wa salamu za rambi rambi kutoka kwa  wakfu wa Emarson zilizotolewa na mwenyekiti wake Said El Gheithy zilisema kwamba wamepokea kwa huzuni taarifa za kifo hicho.

“Kwa hakika tumeondokewa na hatuna jinsi tukubaliane na matokeo hii ni kazi yake Allah haina makosa,lakini alochotuachia Mzee Gora ni urithi mkubwa,”alisema.

Marehemu Haji Gora Haji atakumbukwa kutokana na kazi zake za utunzi wa vitabu vinavyosaidikiwa kumi ambavyo vyengine vinatumika katika skuli mbali mbali nchini Tanzania kikiwemo ‘Siri ya Giningi’ na Kimbunga.

Mbali na vitabu marehemu aliweza kutunga mashairi na nyimbo mbali mbali za taarab, miongoni mwa nyimbo alizotunga ni pamoja na Mpewa hapokonyeki, Kimbuka, Kitendawili, Miujiza na nyengine nyingi.

Marehemu Haji Gora Haji amezaliwa mwaka 1933 amefariki akiwa na umriwa miaka 88 ameacha watoto na wajukuu kadhaa, Allah amsameh makosa yake na amlaze pema peponi.