NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba amesema Pato la taifa la Tanzania lilikuwa kwa asilimia 4.8 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 wa mwaka 2019, licha ya kuwapo kwa mripuko wa ugonjwa wa Covid 19.

Waziri Nchemba, amesema hayo wakati akiwasilisha bungeni hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2020/21  na mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2021/22 jijini Dodoma .

Amebainisha kuwa sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa juu wa mwaka 2020 ni pamoja na sekta ya ujenzi ambayo ilikuwa kwa asilimia 9.1, habari na mawasiliano asilimia 8.4.

Akizitaja sekta nyengine  Mwigulu alisena ni ya  uchukuzi na uhifadhi wa mizigo 8.4, huduma zinazohusiana na utawala 7.8, shughuli za kitaalam 7.3, madini na mawe 6.7, afya na huduma za jamii 6.5.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizokuwa na ukuaji wa uchumi chanya kwani wastani wa pato kwa mtu lilikadiriwa kufika shilingi milioni 2.6 sawa na dola za kimarekani 1151 kwa mwaka 2020, ikilinganishwa na shilingi za Kitanzania milioni 2.5 sawa na dola za Marekani 1118.9 kwa mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.1.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2021/22, shabaha za uchumi ni Kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 5.6 mwaka 2021;  Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 hadi 5.0

katika muda wa kati.

Jambo jengine ambalo alisema ni Mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) kufikia asilimia 15.9 ya

Pato la Taifa mwaka 2021/22 na wastani wa asilimia 16.3 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2023/24.

Alisema eneo jengine ni kuimarisha, Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.5 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 kutoka

matarajio ya asilimia 12.9 mwaka 2020/21 na  Kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa, ili kuendana na makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Suala jengine alisema ni Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).

Alisema katika kuchoche uchumi shindani na shirikishi, msukumo utawekwa katika miradi inayolenga kuwa na utulivu wa uchumi kwa uendelezaji wa reli, barabara, madaraja, usafiri wa majini, anga, nishati, bandari, viwanja vya ndege pamoja na utekelezaji wa mpango kazi wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Amesema katika eneo hilo miradi  itapewa uzito ikiwemo uendelezaji wa miundombinu ambapo amesema mradi wa reli katika mwaka wa fedha 2021/22 kutakuwa na ukarabati wa njia ya kuu za reli, matengenezo ya njia za reli, karakana na majengo ya reli, vichwa vya treni na ukarabati wa mabehewa.

Dk. Mwigulu, amesema msukumo pia utawekwa katika barabara za lami zinazofungua fursa za kiuchumi nchini, barabara za mikoa, barabara ziendazo kasi, barabara za mzunguko jiji la Dodoma, barabara za juu na zile za mijini na vijijini yaani Tarura.

Alisema katika usafiri wa majini Serikali itajenga na kukarabati gati katika maziwa makuu kuboresha bandari zote hasa Bandari ya Dar es Salaam na kwa upande wa usafiri wa anga ni maboresho ya jengo la pili la abiria, kuboresha viwanja vya ndege, Songwe, Msalato na viwanja vingine vya mikoa ya Kigoma, Sumbawanga na Shinyanga.

Serikali alisema pia itaendelea na ujenzi na ukarabati wa barabara zinazounganisha Tanzania na nchi jirani zikiwemo ya Sumbawanga hadi Matai – Kasanga Port (km 117); Isaka – Lusahunga (km 242.2); Nyakahura –16

Kumubuga – Murusagamba na Kumubuga – Rulenge – Kabanga Nickel –

Murugarama (km 141).

Barabara nyengine alizitaja ni ya  Sumbawanga – Mpanda – Nyakanazi (km 432.56); Nyanguge – Musoma na mchepuo wa Usagara (km 202.25); Nyamuswa – Bunda – Kisorya (km107.4); Mwigumbi – Maswa – Bariadi – Lamadi (km 121); Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi (km 341.25); Tarakea – Holili (km 53); Barabara ya Mpemba – Isongole (km 51.2); na barabara ya Geita – Bulyanhulu – Kahama (km 120).

Waziri Mwigulu akizungumzia deni la taifa alisema hadi kufikia Aprili 2021 deni la Serikali lilikuwa limefikia wastani wa Sh60.9 trilioni, ambapo kati ya hizo,  deni la nje lilikuwa Sh43.7 trilioni na deni la ndani Sh17.3 trilioni lililotokana na kupokelewa kwa  mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Dk. Mwigulu alisema taarifa ya tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali iliyofanyika mwaka 2020 ilionyesha kuwa deni la hilo ni himilivu kwa muda mfupi, muda wa kati na pia kwa mrefu.

Akizungumzia mwenendo wa thamani ya shilingi dhidi ya dola za Marekani, Dk Mwigulu amesema   imeendelea kuwa tulivu kwani Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Sh2298.5 Aprili 2021, ikilingansihwa na 2291.3 Aprili 2020.

Alisema  utulivu wa shilingi umetokana na hatua mbalimbali zilizochukuwa na Serikali katika usimamizi wa sera za fedha pamoja  na bajeti katika biashara ya bidhaa na huduma, lakini pia katika  uhamisho wa mali nje ya nchi na mwenendo chanya wa baadhi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.