NA ASYA HASSAN

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kusini,  imetakiwa kubuni vyanzo vipya vya mapato pamoja na kudhibiti matumizi ya mapato ili Wilaya ipige hatua za kimaendeleo.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Rashid Makame Shamsi, alipokuwa katika kikao cha Baraza la Madiwani la Wilaya hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo iliyopo Kitogani Wilaya ya Kusini Mkoa w Kusini Unguja.

Alisema imefika wakati kwa Halmashauri kufikiria vyanzo vipya vya mapato, ikiwemo kuanzisha soko la pamoja la mwisho wa wiki litakalowasaidia wananchi kupata mahitaji yao kwa karibu.

Hata hivyo, Mkuu huyo alisema hatua hiyo itasaidia kutanua wigo na kupata mbinu mpya ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato hayo.

Akizungumzia suala la udhibiti wa mifugo inayoachiwa kiholela alisema halmashauri inatakiwa kuandaa eneo la kuihifadhi mifugo hiyo, ili kuwatoza faini wafugaji wanaoachia mifugo yao kuzurura ovyo.

Alisema kuachiwa kwa mifugo hiyo inapelekea kuwepo kwa changamoto nyingi ikiwemo ya uchafuzi wa mazingira katika vijiji na maeneo ya fukwe pamoja na kuhatarisha usalama kwa waendesha vyombo barabarani.

Katika hatua nyingine Shamsi alisema Wilaya inakabiliwa na tatizo la uharibifu wa mazingira kwa watu kuhamisha rasilimali ya mchanga pamoja na ukataji wa misitu hali inayoleta uharibifu mkubwa na kuikosesha serikali mapato yake.

Hata hivyo, Shamsi alitumia fursa hiyo kuwataka Madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo kudhibiti tatizo hilo ili lisiendelee.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mustafa Mohammed Haji, ambaye pia ni diwani wa wadi ya Muyuni alisema ni jukumu la kila diwani kuwahoji watendaji wa halmashauri juu ya  jambo husika.

Aidha ,aliahidi kuwasimamia watendaji hao kutekeleza majukumu yao ya msingi ikiwemo kusimamia vibali vya ujenzi ambavyo vinaonekana kutokatwa na wananchi wakati wanapojenga.

Nao wajumbe wa baraza hilo wameelezea namna walivyojipanga kwa kuhakikisha wilaya inaimarika katika hali ya kimaendeleo pamoja na usafi huku wakiahidi kuwa wataendelea kusimamia vyema miradi ya kimaendeleo wilayani humo.

Kikao hicho cha Baraza la Madiwani kilijadili utekelezaji wa robo ya mwisho wa mwaka pamoja na kuwasilisha marekebisho ya mapato na matumizi ya halmashauri hiyo kwa mwaka 2021/2022.