NA KHAMISUU ABDALLAH

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, amesema serikali itaendelea kufanya mapitio na marekebisho ya sheria ya mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa kuzingatia maslahi ya watumishi wake.

Alieleza hayo wakati akifungua kikao maalum cha kujadili utaratibu wa kukokotoa mafao ya watumishi kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar kilichofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil, Kikwajuni.

Alisema kuwepo kwa sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii kunalenga kulinda na kuthamini maslahi ya kundi kubwa la wananchi ambao ndio nguvu kazi ya taifa waliokuwepo kazini na wale wanaofikia umri wa kustaafu.

Aidha alibainisha kuwa serikali imekuwa ikifanya marekebisho ya mara kwa mara ya sheria ya mfuko huo inayotokana na sheria namba mbili (2) ya mwaka 1998, ambapo ikafanyiwa tena marekebisho mwaka 2005 na kurekebishwa tena mwaka 2016.

Alisema hatua hiyo inaonesha wazi kuwa serikali imekuwa ikifanya hivyo ili kuhakikisha inalinda maslahi na mafao ya watumishi wake baada ya kumaliza muda wao wa kustaafu wakiwa serikalini au nje ya serikali.

Alibainisha kuwa sheria hiyo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi, malalamiko ambayo yamekuwa makubwa hivyo serikali haina budi kulishughulikia jambo hilo ili kuona mfuko huo unasimama kwa ajili ya wafanyakazi.

Makamu Hemed alibainisha kuwa serikali ya awamu ya nane iliahidi kushughulikia matatizo ya wafanyakazi na makundi mbalimbali hivyo jambo hilo halina budi kufanyiwa kazi ili kuleta maslahi mazuri kwa wananchi na wafanyakazi wake.

Makamu Hemed, alisisitiza kuwa Wazanzibari na wafanyakazi wameona kwenye sheria hiyo kuna mapungufu hivyo ipo haja ya kuangaliwa tena sheria hiyo ili kuendana na hali halisi iliyopo sasa.

Hivyo, aliwashauri washiriki wa mkutano huo kutoa mapendekezo yao kwa uwazi kwa tume hiyo maoni ambayo yataisaidia tume hiyo kupata muelekeo mzuri wa kuwa na sheria bora zaidi itakayoondoa mapungufu yaliyopo sasa.

Wakati huo huo, Makamu Hemed alitoa muda wa saa moja kuhakikisha Makatibu wakuu na Wakurugenzi ambao walitakiwa kushiriki mkutano na kutohudhuria hadi muda wa ufunguzi, kufika ukumbini na kushiriki kikamilifu.

Hivyo alibainisha kuwa serikali haina budi kulifanyia kazi kwa nguvu zote ili kuona mfuko huo unasimamia maslahi ya wafanyakazi wake wanaofikia umri wa ukomo katika utumishi wao serikalini.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alisema tume imeamua kufanya mapitio ya sheria hiyo kutokana na malalamiko kutoka kwa wafanyakazi juu ya mfumo wa kukokotoa maslahi yao pale wanapofikia umri wa kustaafu.

Alisema moja ya kazi ya tume hiyo ni kuangalia sheria zote zinatungwa na pale inapohisi kuwa na haja ya kurekebishwa baada ya kupata maoni ya watu mbalimbali basi sheria hizo zinatungwa kwa ajili ya kusaidia maslahi ya wananchi na nchi kwa ujumla.

Hata hivyo Waziri Haroun alieleza kusikitishwa na idadi ndogo ya Makatibu Wakuu na Wakurugenzi waliohudhuria kikao hicho kwani serikali inafanya mambo hayo kwa maslahi ya wafanyakazi na wananchi lakini baadhi ya watendaji wamekuwa wakidharau jambo hilo.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Khadija Shamte Mzee, alisema tume yake imeamua kutoa elimu katika eneo hilo kwa mafao ya wachangiaji wakati wa kufikia umri wa kustaafu.

Aidha alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alipokutana na uongozi wa ZSSF alisisitiza kuangaliwa upya suala hilo kwa hatma ya watumishi na wanachama wa mfuko huo.