NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameutaka uongozi wa wizara ya Afya kuongeza nguvu katika kitengo cha damu salama kwa kuwaongezea vitendea kazi na kujali stahiki za wafanyakazi ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.

Hemed alieleza hayo katika maadhimisho ya siku ya uchangiaji damu duniani, illiyofanyika huko katika Ofisi za Kitengo cha Damu salama zilizopo Sebleni mjini Zanzibar.

Aliwapongeza wafanyakazi wa kitengo hicho kwa kazi kubwa wanayofanya katika kujitoa kwao kwa moyo mmoja na kuhakikisha wanafikia lengo la ukusanyaji wa damu kwa wingi ili kuokoa maisha ya wenye mahitaji wakiwemo mama wajawazito na watoto.

Alisema kuwa kutokana na suala la uchangiaji damu kumgusa kila mtu katika jamii linahitaji kupewa kipaumbele bila ya kuangalia itikadi za kisiasa, kidini na kikabila.

Makamu wa Pili wa Rais, alimuagiza Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuzingatia kuwaweka kwenye nafasi watu wenye uwezo watakaosaidia kuimarisha kitengo hicho cha damu salama.

Alifafanua kuwa, kumekuwepo kwa tabia isiyoridhisha kwa baadhi ya wakurugenzi katika wizara hiyo kuingilia utendaji kazi wa kitengo jambo ambalo halitoi tija na linawanyima uhuru watendaji waliopo katika kituo hicho.

Akigusia suala la ubunifu, Hemed aliwataka watendaji wanaofanya kazi katika kituo hicho kuwa wabunifu katika kuongeza ufanisi wa kazi badala ya kutegemea bajeti kutoka serikalini.

Aidha, katika maadhimisho hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kwa ushirikiano wanaouonesha hasa wa kuandaa mabonanza ya uchangiaji wa damu.

Pamoja na mambo mengine, Hemed alitoa rai kwa wananchi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu na aliwatoa hofu kuwa suala la uchangiaji damu ni salama ambapo wafanyakazi wanaotoa huduma katika kitengo hicho wana utaalamu, uweledi na umakini wa kutosha.

Naye, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Nassor Ahmed Mazuri alitumia fursa, hiyo kuwashajihisha watu kuendelea kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uchangiaji wa damu ili kuokoa maisha ya watu.

Alieleza kwamba, uzoefu unaonesha uhitaji wa damu Zanzibar ni mkubwa zaidi kuliko kiwango kinachochangiwa akitolea mfano kwa mwaka jana uniti 16,000 zilikusanywa lakini uhitaji wa damu ulifikia kiwango cha uniti 27,000.

Alisema kuna umuhimu wa watu kuendelea kujitokeza kuchangia damu kwani Uniti moja ya mchangiaji ina uwezo wa kuokoa maisha ya watu watatu jambo ambalo lina tija kubwa kwa jamii.