NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali itaendelea kuwahudumua majeruhi waliopata ajali Mkoani Shinyanga iliyotokea Juni 2 mwaka huu.

Hemed alieleza hayo jana alipofika katika hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kuwajulia hali majeruhi hao pamoja na kuwafariji.

Alisema serikali zote mbili zitaendelea kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha afya za majeruhi hao ambao ni watumishi wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar waliokuwa ni wanafunzi wa kada ya afya katika chuo cha Bugema kilichopo   nchini Uganda.

Aliwataka madaktari hospitani hapo kuendelea kuwapatia huduma bora majeruhi hao na serikali kupitia mratibu wake anaesimamia shughuli za serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili Wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi aliopo Dar es Saalam ataendelea kutoa ushirikiano unaohitajika.

Aidha, aliwaagiza madaktari wanaowasimamia majeruhi kutofanya haraka ya kuwatoa wagonjwa mpaka pale watakapojiridhisha kuwa afya zao zimeimarika na serikali itaendelea kugharamia matibabu yao.

“Kamwe isitokee sababu yoyote ile itakayofanya waganjwa wetu kukosa huduma”, alisema Makamu huyo.

Alisema serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefarajika na jitihada zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na madktari katika kuhakikisha afya za majeruhi hao zinaimarika.

Naye daktari bingwa wa mifupa katika hospital ya Taifa Muhimbili, Dk. Victoria Munthali alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais kuwa uongozi wa hospitali hiyo kwa kushirikiana na madaktari wataendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa mpaka pale afya zao zitakapotengemaa sawa sawa.

Kwa upande wao majeruhi wanaopata matibabu katika hospitali ya Muhimbili walimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa wanamshukuru sana, Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi na wasaidizi wake kwa ushirikiano waliowapatia tangu kutokea kwa ajali hadi sasa.

Walisema wanaridhika na huduma wanazopatiwa kutoka kwa madaktari pamoja na wauguzi  na kueleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni kupata maamuzi lakini afya zao zinaendelea kuimarika vizuri.

Makamu wa Pili wa Rais amefika hospitalini hapo akitokea mkoani Dodoma kwenye kikao cha kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM kilichofanyika juzi.