NA KASSIM ABDI, OMPR

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeahidi kuzipa ushirikiano taasisi na kampuni binafsi zenye lengo la kuunga mkono jitihada za kuitambulisha historia ya Zanzibar kwa lengo la kuimarisha utalii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo wakati akizindua vipindi vya kumbukumbu ya mambo ya kale Zanzibar vilivyopewa jina ‘SOGEA NIKUJUZE’ uzinduzi ambao uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil uliopo Kikwajuni jijini Zanzibar.

Hemed aliwapongeza watayarishaji wa vipindi hivyo vilivyoandaliwa na kampuni ya Mavips Pictures kwa ushirikiano wa pamoja na Mambo TV Swahili, kwa kujitokeza kuwa wa kwanza kuja na wazo la kutayarisha vipindi maalum vya kuitambulisha historia ya Zanzibar.

Alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuitangaza historia ya Zanzibar, hivyo alitoa rai kwa vyombo vyengine vya habari kuiga mfano huo kwani historia ya Zanzibar ina uwanja mpana.

Alieleza kuwa, jumuiya na taasisi binafsi zinapaswa kushiriki lengo likiwa ni kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha uendelezaji wa utalii wa ndani na nje akitolea mfano viongozi wa dini wana mchango mkubwa wa kutoa elimu kwa kuizungumzia historia ya Zanzibar kwa kuinasibisha na dini ya kiislamu.

Hemed alisema Zanzibar ina maeneo mengi ya kihistoria ambayo yalikuwa sehemu ya uchumi wa nchi na kueleza kuwa historia ni roho ya taifa kwani inasadia kutengeneza njia sahihi za maisha na kujua wapi tunapoelekea.

Alisema Zanzibar imejaaliwa kuwa na vivutio vyingi vya utalii kushinda nchi nyingi duniani lakini changamoto inayojitokeza baadhi ya historia hizo hazijulikani na wazawa jambo linalorejesha nyuma kukuza kasi ya uchumi na kujenga ustawi mzuri wa jamii.

Alifafanua kuwa, uchumi wa Zanzibar ya kale ulikuwa na vyanzo vya kuaminika kutokana na miundombinu imara iliyowekwa akitolea mfano rasi ya Mkumbuu iliyoko Pwani ya Magharibi ya Pemba kuanzia mapema mwa karne 10 ilikuwa ni bandari iliyostawi kwa kusafirisha biashara zilizopelekwa nchi mbali mbali barani Afrika, Uarabuni, India na Ghuba ya Uajemi.

Aidha alisema rasi ya Mkumbuu ilikuwa kituo muhimu cha kuenea kwa dini na biashara zama hizo kabla ya ujio wa utawala wa kwanza wa kigeni wa kireno uliotajwa katika rekodi za Oman ulioanzia karne ya nane.

Pamoja na mambo mengine, alieleza kuwa, uchunguzi wa akiolojia uliofanyika kwenye mapango ya Fukuchani Mkoa wa Kaskazini Unguja na Kuumbi Jambiani umebaini kuwa Zanzibar katika karne ya kwanza ilikuwa tayari imeanzisha uhusiano wa kibiashara na nchi za bara Arabu, India na Afrika.

“Kinachohitajika sasa ni kuanzisha fursa nyingi kwa wazanzibari katika kuitangaza zaidi historia kwa lengo la kuhamasisha watalii wa ndani waweze kutembelea maeneo ya kihistoria kwa ajili ya kujifunza mambo mbali mbali”, alisema Makamu wa Pili.

Hemed alisema kuna haja kwa jamii kubadilisha mtazamo katika kuendeleza utalii wa ndani kwa kuondosha dhana kuwa maeneo ya kiutalii ni Mji Mkongwe, Jozani, Kizimkazi na kwenye mashamba ya viungo.

Naye, waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Leila Mohamed Mussa aliwapongeza vijana wa kampuni ya Mavips Picture kwa kujitolea na kuthamini azma ya serikali ya awamu ya nane katika kukuza sekta ya utalii kwa kuendeleza historia ya Zanzibar kwa kufanya ubunifu wa kuandaa vipindi.

Alieleza kuwa, vijana hao wameonesha utayari kwani hadi sasa wamekwisha andaa vipindi vya kurushwa hewani kwa kipindi cha mwaka mzima jambo ambalo linaashiria kujipanga vyema katika kutoa elimu kupitia vipindi hivyo bila ya kusita.

Leila alitumia fursa hiyo kwa kuwaomba vijana na kampuni nyengine kuiga mfano wa kampuni ya Mavips Pictures kwa kujitokeza kubuni vipindi kama hivyo ili kujenga mioyo ya kizalendo katika kulitumikia taifa lao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mavips Pictures, Mudrik Kassim alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa vipindi vilivyoandaliwa vina lenga kutanua wigo kwa wenyeji na wageni kufuatilia historia ya Zanzibar.

Mudrik alieleza kuwa kutangazwa kwa vipindi hivyo, kutatoa muamko wa kuimarishwa miundombinu ya burudani ambapo utaratibu wa vipindi vitarushwa hewani kupitia Mambo TV Swahili kila siku ya Jumamosi wakati wa saa 2:30 usiku kuanzia Juni 12 mwaka huu.

Alieleza kwamba mbali na mafanikio waliyoyapata katika kutayarisha vipindi hivyo lakini walikabiliwa na changamoto ikiwemo ufinyu wa bajeti katika kuyafikia maeneo mengi ya kihistoria.