Awahakikishia mazingira rafiki wawekezaji

NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali imedhamiria kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda ili kutatua changamoto ya ajira inayowakabili vijana.

Makamu huyo alieleza hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua eneo maalum la viwanda vidogo liliopo Amani, ambapo alisema viwanda vina mmchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na kupunguza ajira.

Alisema serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi imeamua kuweka mkazo katika sekta ya uwekezaji kwa kuwakaribisha wawekezaji kuekeza katika eneo la viwanda.

Wakati akitembelea maneo mbali mbali ya eneo hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, aliwahakikishia waekezaji waliopewa nafasi katika eneo hilo kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano unaostahiki.

Hemed aliwashauri wawekezaji hao kuweka mazingira mazuri ya kazi zao kwa kuajiri watu muhimu watakaotoa msaada kwa wamiliki wa viwanda hivyo akitolea mfano kuajiriwa kwa mtu wa rasilimaliwatu pamoja na wahasibu kutasaidia kuweka sawa majukumu ya kazi.

Katika ziara yake hiyo Makamu wa Pili wa Rais aliwasisitiza wawekezaji waliopewa nafasi katika eneo hilo kwamba serikali ya awamu ya nane sio haiamini kwenye kodi kubwa hivyo kiasi ambacho wanapaswa kulipa wahakikishe wanalipa kwa wakati.

“Serikali hii ni muumini wa kodi ndogo hivyo nawaomba sana ndugu zangu wawekezaji kusiwe na visingizio katika suala la ulipaji wa kodi kwa serikali”, alisema.

Aidha, Hemed aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar kupitia upya sheria ya viwango vya kodi ili kila muwekezaji aweze kufahamu kiwango cha kodi anayostajiki kulipia bila ya kuathiri upande wowote.

Makamu wa Pili Rais alieleza faraja yake kwa jitihada nzuri zinazochukuliwa na uongozi wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar katika kuhakikisha wawekezaji wanapewa maeneo ndani ya kipindi cha muda mfupi jambo ambalo linaashiria utayari kwa kuondoa urasimu na kuyafanyia kazi maelekezo ya Rais Dk. Mwinyi.

Akifanya majuumuisho baada ya ziara hiyo Mhe. Hemed alionesha kutoridhishwa na baadhi ya mazingira katika eneo hilo kwa kufanywa jaa la kuhifadhia vifaa vilivyopitwa na wakati nakuahidi kuwa serikali itatoa maamuzi ndani ya kipindi cha muda mfupi.

Aliuagiza uongozi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja Bodi ya Mapato Zanzibar kuangalia upya taratibu za ulipaji wa kodi ili kuepusha serikali kupoteza mapato yake kutoka kwa waekezaji.

Makamu wa Pili wa Rais aliwathibitishia wawekezaji wapya waliopewa maeneo hivi karibuni kuwa serikali inawakaribisha na wasisite kuwasilisha changamoto zozote zinazowakabili katika utendaji wa kazi zao.

Nae, Mkurugenzi wa Mamlaka ya kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Sharif Ali Sharif alimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa ziara yake hiyo ambayo imekuwa ni chachu kwa mamlaka hiyo katika kufanyakazi kwa bidii ili kuyafkia malengo ya serikali.

Sharif alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa maelekezo aliyoyatoa watahakikisha wanayachukulia hatua kwa ushirikiano kati ya Mamlaka hiyo na wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Uchumi na Uwekezaji.

Nao wawekezaji wa waliopewa nafasi ya kuekeza katika eneo hilo la viwanda vidogo wameipongeza serikali kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ambayo yamewasaidia kuendesha kazi zao bila ya usumbufu.