HATIMAYE rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amehukumiwa kifungo cha miezi 15 jela, hatua hiyo inafuatia kupuuza amri ya mahakama ya kumtaka afike mbele ya tume maalum inayochunguza madai chungunzima yanayomkabili ya rushwa enzi ya utawala wake.

Mahakama ilikuwa na jukumu la kuamua kama Zuma anapaswa kuadhibiwa kwa kukataa wito wa mahakama na amri ya mahakama ya kumtaka afike mahakamani kutoa ushahidi kuhusu shutuma za rushwa wakati wa utawala wake.

Hukumu hiyo iliyotolewa na kaimu jaji mkuu wa Afrika Kusini, Sisi Khampepe bila ya Zuma mwenyewe kuwepo mahakamani ni ya kwanza katika hisotria ya taifa hilo kwa rais mstaafu kuhukumiwa kifungo gerezani.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwenyekiti wa kamati maalum ya uchunguzi wa mahakama, Raymond Zondo ambayo imekuwa ikichunguza madai hayo aliiomba mahakama itamke kuwa rais huyo wa zamani alidharau mahakama na imhukumu kifungo cha miaka miwili.

Jaji Khampepe alisema kwamba Zuma ametiwa hatiani kwa kosa la kutoheshimu na kuipuuza mahakama baada ya kushindwa kutii amri ya kufika mbele ya tume ya mahakama inayochunguza madai ya rushwa, uhujumu wa taifa na udanganyifu enzi ya utawala wake.

“Aina hii ya kutokujali na kukashifu ni kinyume cha sheria na lazima adhabu itolewe, Khampepe alisema. Nimeachwa bila chaguo jengine, isipokuwa kumhukumu Zuma kifungo, na ni matumaini kwamba kufanya hivyo kunapeleka ujumbe bila shaka, utawala wa sheria na usimamizi wa haki unashinda”,alisema jaji huyo.

Uamuzi huo umetolewa na mahakama ya katiba ambacho ndicho chombo cha juu zaidi cha utoaji haki nchini Afrika Kusini na kushindwa kwa Zuma kufika mbele ya tume iliyoundwa na mahakama kumetajwa kuwa ni kitendo cha dharau kubwa iliyochupa mikapa.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Khampepe alisema “Jacob Zuma anahukumiwa kifungo cha miezi 15. Zuma anaamriwa kujisalimisha mwenyewe kwenye kituo chochote cha polisi cha Afrika Kusini au cha mjini Johannesburg ndani ya siku tano tangu kutolewa kwa amri hii”.

Itakumbukwa kuwa tangu mwanzo Zuma alikwishaeleza kutokuwa tayari kufika mbele ya tume ya mahakama ambayo hadi sasa imekwishasikiliza ushahidi unaomuhusisha moja kwa moja kiongozi huyo wa zamani na makosa kadhaa.

Kupitia barua yake yenye kurasa 21 aliyomuandikia jaji mkuu wa Afrika Kusini, ambayo mahakama imeitaja kuwa ni ya fedheha, Zuma alidai kwamba yupo tayari kwenda jela, lakini siyo kujieleza mbele ya tume hiyo.

Katika barua hiyo ambayo Zuma aliiweka wazi kwa umma, akidai kwamba mwenyekiti wa tume hiyo ambaye ni naibu jaji mkuu Raymond Zondo hatomtendea haki na kwamba ushahidi uliowasilishwa dhidi yake umechochewa kisiasa.

Hukumu hiyo iliyotolewa kwa rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini inaonesha ni mwanzo wa safari ya muda mrefu wa kiongozi huyo atakavyomaliza maisha yake hapa duniani akiwa jela.

Miezi 15 jela aliyohumiwa bado haija husisha hukumu za kesi zake zilizopo mahakamani ambapo anakabiliwa na mashitaka 16 ya ufisadi aliyoyafanya wakati huo akiwa madarakani kama makamu wa rais.

Akiwa makamu wa rais wa wakati huo chini ya rais Thabo Mbeki, Zuma anatuhumiwa kwa kupokea rushwa ya randi 500,000 sawa na dola 35,000 kwa mwaka kutoka kwa kampuni ya Thales.

Fedha hizo alizopokea kuanzia mwaka 1999 zilikuwa mahusi kwa kutumia nafasi yake aikingie kifua kampuni hiyo dhidi ya uchunguzi wa mikataba, baada ya ufichuzi uliotolewa bungeni. Hata hivyo kampuni hiyo inayakana madai hayo.

Aidha Zuma anahusishwa na kashfa manunuzi hayo ya ndege za kivita, boti za doria na vifaa vya kijeshi katika kampuni tano za Ulaya, zilizokuwa na thamani ya randi bilioni 30 ambayo ni sawa na karibu dola bilioni 2.5.

Wakati wa utawala wake akiwa kama rais wa Afrika Kusini, alihusishwa kuisaidia familia ya wafanyabishara nchini humo inayojulikana kama Gupta ambapo wlaipata kandarasi mbalimbali za upendelea wakisaidiwa na rais huyo.

Baadhi ya mawaziri wa zamani, maofisa wa ngazi ya juu wa serikali na wakuu wa mashirika ya umma ni miongoni mwa wale waliotoa ushahidi unaomuhusisha Zuma na kashfa chungunzima za rushwa.

Wengi wamesema wamesema kwamba wakati akiwa rais Zuma aliruhusu baadhi ya watu kutoka familia ya Gupta inayohusishwa na kashfa kadhaa nchini Afrika Kusini kushinikiza uteuzi wa mawaziri na hata namna ya kufikiwa kwa mikataba ya fedha nyingi kwenye kampuni za umma.

Akiwa madarakani kati ya mwaka 2009 na 2018, Zuma alishinikizwa na chama chake cha ANC kujiuzulu kufuatia ongezeko la msururu wa kashfa na tuhuma za ufisadi.

Tangu alipojiuzulu mnamo mwaka 2018, Zuma amekuwa akifika mahakamani akikabiliwa na shutuma za ufisadi ambazo amekuwa akizikanusha, hadi kupewa hukumu hiyo ya kukataa kuhudhuria mahakamani.

Wakati mmoja alipohudhuria mahakamni nje ya jengo la mahakama, Zuma aliwaambia wafuasi wake kwamba madai dhidi yake yanachochewa kisiasa na wale aliowaita kuwa ni wabaya wake.

Wafuasi wake walifurika kwa wingi mahakamani kuonesha kumuunga mkono akiwemo katibu mkuu wa ANC, Ace Magashule ambaye inasemekana ni mfuasi kidakindaki wa Zuma.

Zuma alionekana kupata pigo kufuatia katikati ya kesi hizo zikiendelea mawakili wake wote walijiuzulu bila ya kutoa maelezo yoyote, na kuteua wakili mpya Thabani Masuku.