NA MAULID YUSSUF, WEMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali amewaeleza wafanyabiashara nchini Uturuki kwamba Zanzibar imefungulia milango na kuwakaribisha nchini kutumia fursa za uwekezaji.

Jamal alieleza hayo akiwa na waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohammed Said walipokutana na jumuiya ya wafanyabiashara katika jiji la Istanbul nchini Uturuki ambao wako ziarani nchini humo.

Jamal aliwaeleza wafanyabiashara hao kwamba serikali ya awamu ya nane imejipanga kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kwamba Zanzibar ina fursa nyingi za uwekezaji hivyo ni vyema wakatumia nafasi hiyo.

“Zanzibar imefungua milango kwa kukaribisha wawekezaji kutoka nje kupitia utaratibu wa ushirikiano wa kibiashara kati ya serikali na mashirika binafsi, hivyo tunawakaribisha mje muangalie fursa”, alisema waziri huyo.

Aidha waziri huyo alilieleza shirikisho hilo kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka miradi ya kimkakati kwa ajili ya kutekeleza mapinduzi ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi pamoja na ujenzi wa viwanja vya ndege.

“Kwa wakati huu serikali ya Mapinduzi inaimarisha mazingira ya uwekezaji ili yawe rafiki kwa wafanyabiashara wanaowekeza miradi yao visiwani Zanzibar” alisema waziri huyo.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka nchini Uturuki, Zeki Guvercin aliwaomba mawaziri hao kuwapatia taarifa muhimu zinazohusu maeneo ya uwekezaji ya Zanzibar pamoja na namna ya mazingira rafiki ya uwekezaji ili wafanye maamuzi sahihi.

Pia alieleza kuwa wapo tayari kutoa mashirikiano katika masuala ya biashara pamoja na kwamba wapo tayari kuwaunganisha na kampuni maarufu za wafanyabiashara ambayo wana nia ya kufanya biashara na uwekezaji katika maeneo ya kimkakati ya uwekezaji visiwani Zanzibar.

Wakati huo huo, waziri Jamal na Simai wakiendelea na ziara yao nchini humo walitembelea Chuo cha Mafunzo ya Amali cha Uturuki Haydar Pasa Mesleki ve Teknik Anadolu Lisesi na kukubaliana kufanya uwezekano wa kubadilishana wanafunzi kwa lengo la kujifunza masuala mbalimbali ya Amali kati ya Zanzibar na Uturuki.