NA MARYAM HASSAN

ALIYEBA madafu sita yenye thamani ya shilingi 6,000 amehukumiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mwaka mmoja.

Mbali na kutumikia adhabu hiyo, mshitakiwa huyo ametakiwa kulipa faini ya shilingi 6,000 na fidia ya kiwango kama hicho cha fedha, akishindwa atumikie Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita.

Hakimu wa mahakama ya mwanzo Mwera Abubakar Suleiman Thabit, ametoa adhabu hiyo kwa mshitakiwa Mohammed Khamis Haji (27) mkaazi wa Tunguu wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Hakimu huyo alisema, ameamua kutoa adhabu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.

Kabla ya kupewa adhabu hiyo mshitakiwa aliiomba mahakmaa kumpunguzia adhabu, kwa sababu ana familia inamtegemea.

Mapema, wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Muzne Mbwana Suleiman, aliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria.

Aidha alisema, hana kumbukumbu ya makosa ya nyuma dhidi ya mshitakiwa huyo, hivyo mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa uzito wa kosa aliloshitakiwa nalo.