LYTTON, CANADA
POLISI nchini Canada imesema joto limesababisha vifo mashariki mwa taifa hilo, ambapo katika saa 24 kumetokea vifo vya ghafla takribani 25.
Katika eneo la Lytton kiwango cha joto kimeripotiwa kufikia nyuzi joto 47.9, kikitajwa kupindukia rekodi ya taifa hilo iliyowekwa katika mji wa Saskatchewan mnamo mwaka 1937.
Katika wimbi hili la sasa la joto, maeneo mengi ya upande wa Amerika ya Kaskazini yameripoti kiwango cha juu cha joto kinachopindukia nyuzi joto 40, likiwemo jimbo la Oregon, magharibi mwa Marekani.
Polisi wa British Columbia wamepokea taarifa za vifo tangu Jumatatu, vifo vingi vikijumuisha wazee, ambapo wanasema kiwango hicho cha joto kupiga katika eneo hilo kilisababisha vifo hivyo.
Hapo juzi kiwango cha joto nchini Canada kiliongezeka zaidi ikawa siku ya tatu mfululizo -ilikuwa nyuzi joto 49.5 huko Lytton, British Columbia, ambapo kabla ya wiki hii kuanza kiwango cha joto cha Canada hakikuwahi kuvuka nyuzi joto 45.
“Waangalie majirani zako, familia yako pamoja na wazee unaowajua,” Polisi wa Canada Mike Kalanj, ambaye yuko Vancouver wilaya ya Burnaby, alisema.
“Hali ya hewa inaweza kuwa hatari kwa jamii ya watu ambao hawajiwezi hasa wazee na wale wenye matatizo ya kiafya,” aliongeza. Ni muhimu tukawajulia hali kila mara.”
Kwa mujibu wa polisi, joto hilo linaaminika kuwa limesababisha vifo vya watu 69 katika mji wa Vancouver wilaya ya Burnaby. Wengi wakiwa wazee na waliokuwa na matatizo ya kiafya.
Katika kijiji cha Lytton, mkazi wa eneo hilo Meghan Fandrich amekiambia chombo cha habari cha Globe & Mail kuwa ilikuwa vigumu hata kutoka nje.