KIGALI, RWANDA

RAIS wa Rwanda Paul Kagame, amesema nchi hiyo inaweza kurejeshwa tena kwenye karantini ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa corona.

Kauli ya rais huyo imekuja kufuatia taarifa ya wizara ya afya nchini humo, kueleza kuwa kuna ongezeko la visa vya maambukizi ya corona pamoja na kwamba chanjo ya ugonjwa huo inatolewa.

Rais Kagame aliwahimiza wananchi nchini humo kuhakikisha wanachukua tahadhari ili kuepuka kasi ya maambukizi na kwamba kama kutaonekana kasi ya maambukizi kuwa juu nchi atairejesha tena katika karantini.

Kagame alisema kuongezeka kwa kasi ya maambukizi ya corona inaonekana kama vile kunataka kujitokeza wimbi la tatu la maambukizi ya ugonjwa huo nchini humo, lakini tahadhari zitachukuliwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya afya nchini humo, katika siku saba zilizopita maambukizi ya corona yameongezeka kufikia watu 1,307 kutoka watu 334 kabla ya wiki moja huku vifo vya watu 12 vikiripotiwa.

Zoezi la utoaji wa chanjo ya corona nchini humo linaendelea ambapo zaidi a watu 390,000 wameshapatiwa chanjo, huku wengine wakipatiwa chanjo hiyo kwa mara ya pili.

Waziri wa afya Daniel Ngamije, alisema lengo la taifa hilo ni kuwapatia chanjo ya corona watu milioni ifikapo mwakani, huku akisisitiza wananchi wa taifa hilo kuhakikisha wanajitahidi kuchukua tahadhari ya kujikinga.