KAMATI ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi imezisisitiza wizara mbali mbali za serikali kuwa makini katika kuandaa takwimu zinazohusiana na taarifa za bajeti ili kueka ufanisi wa matumizi ya fedha za umma.

Akisoma hotuba hiyo, Mwenyekiti Ali Suleiman Ameir, alisema tatizo hilo limeonekana kujitokeza kwa Wizara mbali mbali .

Alisema kutokua na takwimu sahihi za taarifa za bajeti kunapelekea kutokua na ufanisi wa matumizi ya fedha za umma lakini pia hazitokua na mipango inayokisi uhalisia wa fedha.

Aidha, kamati hiyo imeridhishwa na ufafanuzi uliotolewa katika changamoto ya upatikanaji wa maji na kushauri Serikali kuhakikisha fedha zilizotengwa katika miradi ya maendeleo kwa mwaka huu zinapatikana kwa wakati.

Pia kamati iliitaka Wizara ya Fedha na Mipango kushirikiana na Wizara ya Maji, Nishati na Madini kueka sawa taarifa za mradi huo ili kuondosha utata uliojitokeza .

Hata hivyo Ali, alibainisha kuwa kamati inaishauri Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, iwapo itatumia fedha za mfuko mkuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo basi fedha zipelekwe moja kwa moja kwa mkandarasi badala ya kupitia katika Wizara hiyo.

Alisema Wizara na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango inapaswa kuripoti taarifa za utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia kuwa wao ndio walioidhinishiwa fedha hizo.

Mwenyekitu huyo aliwakumbusha Mawizara pamoja na watendaji wa Wizara na taasisi zote za Serikali kwamba bajeti zilizoidhinishwa zinapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia malengo ya ilani ya Chama cha Mapinduzi(CCM), dira ya maendeleo ya Zanzibar 2050 na ahadi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi .

Sambamba na hayo aliwaomba wajumbe wenzake wa Baraza hilo kwamba wana wajibu wa kulisimamia hilo ili kuhakikisha yanayotekelezwa na vyombo vya Serikali yanakwenda sambamba na miongozo ya nyenzo hizo muhimu katika utekelezaji wa bajeti hiyo.