NA MARYAM HASSAN

MWENYEKITI wa Kamati ya Maendeleo ya jimbo ambae pia ni Mwakilishi wa jimbo la Mwera, Mihayo Juma Nh’unga, amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuzitumia vyema fedha za mfuko wa jimbo ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo katika kikao cha kutathmini hali ya maendeleo ya jimbo hilo.

Alisema fedha hizo zimelenga kutumika katika sekta ya elimu kwa kutatua uhaba wa madarasa ambayo mengi yao ni mapya yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.

Alisema sekta ya elimu ni muhimu katika nchi hivyo endapo itakuzwa na kuthaminiwa kuna uwezekano wa kupata wataalamu wazuri katika siku za usoni.

Hivyo aliwahakikishia wananchi hao kuwa atazidi kutoa ushirikiano ili kufikia malengo yaliyowekwa ikiwemo kupatikana kwa elimu bora kwa kila mtoto wa jimbo hilo.

Aidha alisema katika jimbo hilo skuli nyingi zinakabiliwa na uhaba wa madarasa na ofisi za walimu lakini kwa kuanza watajenga skuli ya Mtopepo kwa kukamilisha madarasa sita ambayo awali yalijengwa kwa nguvu za wananchi.

“Kama tutajenga kitu ambacho mwakani hakitafanya kazi basi nguvu yetu itakuwa bado haijafanya kazi, hivyo ni vyema tukawa waangalifu katika matumizi yetu,” alisema Nh’unga.

Aidha ili kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa vyema, alisema hadi mwezi Januari mwakani watahakikisha maeneo mengine yakiwemo ya skuli ya Kianga, Mtoni Kidatu  na Masingini yawe yameanza kusomewa.

Kwa upande wake, Diwani wa viti maalum, Khaitham Mwadini Khamis, alisema kamati yao imeweka kipaumbele cha elimu kwa sababu ndio changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa jimbo hilo.

Naye Sheha wa Kianga, Juma Issa Juma, alisema shilingi Milioni 20 za mfuko wa jimbo zilizotolewa watahakikisha zinatumika ipasavyo ili kuongeza kasi ya maendeleo jimboni humo.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa CCM jimbo la Mwera, Mohammed Ameir, alisema kipaumbele kilichowekwa ni mambo yaliyotiliwa mkazo na ilani ya uchaguzi ya chama hicho hivyo viongozi hao hawana budi kusimamia utekelezaji wake sambamba na ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni.

Alisema awamu ya pili watahakikisha skuli ya Masingini ambayo ina madarasa 16 ambayo bado hayajamalizika na kwamba hatua za haraka zitachukuliwa kwa kuwa fedha zilizotolewa haziwezi kujenga madarasa yote hivyo aliwataka wananchi kuwa na subra.