NA MADINA ISSA

KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, CP Mohammed Haji Hassan, amesema tangu mwezi Januari hadi Mei mwaka huu ajali pamoja na vifo vinavyotokana na usafiri wa bodaboda Zanzibar vimeongezeka kutokana na waendesha usafiri huo kutofuata sheria za barabarani.

Kamishna huyo alieleza hayo, katika mkutano na waendesha bodaboda wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Unguja huko katika kiwanja cha Kijangwani Mjini Unguja.

Alisema lengo la kukutana na wafanyabiashara hao ni kujadili jinsi ya kupunguza ajali za barabarani na kuepusha vitendo vya kihalifu ambapo kwa sasa vimeshika kasi.

Alisema katika kipindi hicho jumla ya ajali 93 zimetokea kati ya hizo ajali 34 zimesababishwa na usafiri wa bodaboda vifo kulikuwa na vifo 41 ambapa kati ya hivyo vilivyosababishwa na bodaboda ni 25.

Akizungumza idadi ya watu waliofariki, Kamishna Muhammed, alisema kuanzia Januari hadi Mei waliofariki walikuwa 74 kati yao 27 walikufa kutokana na usafiri wa bodaboda ampapo kwa upande wa majeruhi ni 113 ambapo kati yao 35 wamejeruhiwa kutokana usafiri wa bodaboda.

Alifahamisha kuwa mbali na ajali hizo pia waendesha bodaboda wanajihusisha na vitendo vya kihalifu vikiwemo wizi na ujambazi wa kupora mali za wananchi.

Hivyo, aliwataka madereva hao kuacha mara moja tabia hiyo kwani inawatia hofu wananchi kutumia usafiri huo ambapo wananchi wamekuwa wakiripoti katika vituo vya polisi.

Sambamba na hayo, aliwataka wafanyabiashara hao, kujitathmini na kuhakikisha wanafuata sheria na kanuni za usalama wa barabarani ili kulinda usalama wa raia wanaowapakia pamoja na kupunguza ajali za barabarani.

Nao waendesha bodaboda walisema ajali nyingi zinazotokea katika maeneo mbalimbali zinasababishwa na baadhi ya madereva kuendesha vyombo wakiwa wamelewa hali inayopelekea kuhatarisha usalama wa raia.

Sambamba na hayo, alisema kuwa kumekuwepo mtindo wa baadhi ya wenye gari na kuwapelekea gari zao bodaboda kitendo ambacho kinasababisha kutokea ajali zilizokuwa sio za lazima.