NA MWANTANGA AME

WIKI iliyopita ilikuwa ni siku ya Mazingira Duniani, ambayo iliadhimishwa katika mataifa mengi ikiwemo na Zanzibar.

Siku hii imeadhimishwa kwa kufanyika shughuli mbali mbali za utunzaji wa mazigira, ikiwa ni sehemu ya kuikumbusha jamii wajibu wao wa kuhifadhi, ili hali ya uchagfuzi isiwe endelevu.

Ndio maana leo hii si jambo la ajabu kuona katika maadhimisho hayo yanapofanyika kumekuwa na harakati nyingi za upandaji wa miti katika maeneo mbali mbali ya visiwa hivi vya Unguja na Pemba.

Mfano halisi katika mwaka huu wananchi wa baadhi ya majimbo wameonesha umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti 500, huku sehemu nyengine nayo imepandwa kwa kiwango tofauti.

Hatua hiyo ni ya kupendeza na ni ya kuungwa mkono, kwani itakuwa imeenda sambamba na kauli mbiu ya kimataifa  inayotaka ‘TURUDISHE MAENEO YALIOHARIBIKA  YARUDI KATIKA UASILI WAKE’ huku ya Zanzibar ikiwa  ‘TUNZA MAZINGIRA, DUMISHA UASILI WAKE, KUFIKIA UCHUMI WA BULUU’

Kauli mbiu hizi zinakuja ikiwa ni sehemu ya kuona uhalisia juu ya utunzaji wa mazingira, kwani kila mwaka hutengwa miti ya kupandwa katika maeneo mbali mbali ya visiwa hivi vya Unguja na Pemba.

Wakati utekelezaji wa mpango huo ukiendelea, lakini kuna haja ya kujiuliza kama utaratibu huo unafanyika kwa uhalisia, kwani kila mwaka hutengwa miti ya kupandwa lakini baada ya hapo haieleweki kama inakuwa katika usimamizi mzuri, ili kuona ukuwaji wake ukoje.

Hii ni kutokana na miti hii ikiangaliwa wakati wa kuendesha kampeni hizi za upandaji wake hutumika fedha nyingi kwa ajili ya kuipata na kufanyika zoezi hilo lakini bado hakuna kinachofanyika baada ya hapo.

Hali hiyo imeanza kuonyesha wasi wasi ndani ya jamii kuona kama kuna ukweli wa kile kinachofanyika, kwani baadhi ya watu ndani ya jamii wanajiuliza kiwango cha miti inayotajwa kupandwa ndani ya visiwa hivi  kungeshakuwa na mabadiliko.

Leo hii taarifa ziliopo katika jamii na serikali kwamba visiwa hivi vinakabiliwa na hali mbaya ya kimazingira kutokana na miti mingi kukatwa ovyo, huku kukiwa na kampeni zinazoendesha na serikali na jumuiya binafsi za kupanda miti hasa siku hii ya mazingira duniani.

Kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa inahitajika kufanyika tathmini ya kuona ukweli uko wapi, kwani bado hali ya mazingira inaelezwa haiko vizuri, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa.

Hilo ni jambo la msingi kutokana na fedha zinazotengwa kwa ajili ya kukidhi kampeni hizo, zinaonekana bado haziendi sambamba na kile kinachoelezwa kwani huwa nyingi lakini idadi ya miti inayopandwa ni kidogo na ikizingatiwa huwa miche tuu ambayo bei yake hutakiwa iwe ndogo.

Hii ni kutokana na miti inayopandwa idadi yake hutajwa huwa ni kubwa, lakini inayoonekana wakati kampeni hizo zikifanyika huwa ni michache na zoezi lake huwa halichukui eneo kubwa la kufanyika kwake.

Hali hii, inaonesha wazi kuwa kiwango cha miti inayotangazwa bado ni kitendawili kinachokosa mteguzi, kwani hakuna tathimini inayofanywa kwa vile mingi yake ikishapandwa huwachwa ikue yenyewe.

Hiyo imekuwa ikisababisha miti mingi baada ya kupandwa hufa na kuiafanya nchi hii kutoonekana kuwa na mabadiliko licha ya kampeni hizi kufanywa kila mwaka.

Ndio maana leo hii si jambo la ajabu kuona wafanyaji wa tathmini wanaendelea kutumia ripoti za miaka iliyopita kuelezea hali halisi ya mazingira ya visiwa hivi vya Unguja na Pemba, wakati kube uhalisia kwa baadhi ya miaka kuwepo kwa mabadiliko.

Inawezekana hayo yakiwa yanatokea kutokana na kwamba mradi wa kupanda miti huwa ni endelevu kwa vile vyombo vinavyohusika na uandaaji ya kampeni hizo hutakiwa kutenga fungu maalum za kushughulikia suala hilo.

Baya zaidi katika utengaji huo wa fungu la kununulia miti hiyo kila mwaka, huongezeka kiasi ambacho huonekana gharama kubwa zinazotumika lakini faida ni ndogo.

Kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa kampeni hizo zinaonekana kama mzigo unaotumiwa kwa ajili ya kujinufaisha binafsi, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa vyema.

Suala hilo linahitaji kuangalia kutokana na kuwapo kwa sababu mbali mbali za mitazamo ghasi katika kuendesha kampeni hizo, kiasi ambacho tayari baadhi ya wanajamii kuona hakuna ukweli.

Hiyo huenda ikasababisha ushiriki wa wanajamii kuwa mdogo wakati kampeni hizi zinapofanyika na kujikuta zinaendeshwa na wanajumuiya peke yao bila ya ushiriki wa wananchi.

Hali hii, ikitokea itachangia kuwafanya wanajamii kuona wao hawapashwi kushiriki katika kampeni hizo, jambo ambalo linachangia kuwafanya wenye mitazamo ya kuwa wao sio miongoni mwa wanaotakiwa kuitunza miti hiyo.

Nafikiri imefika wakati, hatua hizi zikaangaliwa kwa undani juu ya suala la kampeni hizi za kupanda miti, ili ziendane ya ukweli halisia kwani bado ushawishi wake ni mdogo.

Hiyo ni kutokana na kuona kampeni hizo mara nyingi hufanyika katika maeneo yale yale yaliofanyika mwaka jana na unaofuata hujirejea, kiasi ambacho hakionekani kuwapo mabadili ya uhiishaji wa mabadiliko ya mazingira.

Hivyo basi, ipo haja kwa taasisi zinazohusika na usimamiaji wa mazingira zikaiona hali hii, na kufikiria njia mpya za kulinda haya mabadiliko tabianchi yasipate nafasi, kwani mfumo unaoendelea kutumika bado haujawa ndio muarubaini wa kumaliza hilo.

Hilo ni kutokana na kampeni zinaendelea kupanda miti lakini kunakosekana uangalizi baada ya kupandwa kiasi ambacho zinaonekana hazizai matunda huku kukiwa na wasi wasi wa idadi kubwa ya miti inayodaiwa kupandwa kufikia uhalisia.

Jambo la kujiuliza hivi nasari zetu zina uwezo wa kuzalisha miche zaidi ya milioni moja ama 5000, nafikiri kunahitaji ukweli wa kuliangalia hili ili kuwe na mbinu  bora zitazoweza kusaidia kutekeleza vyema ujumbe wa mwaka huu.

‘TURUDISHE MAENEO YALIOHARIBIKA  YARUDI KATIKA UASILI WAKE’ huku ya Zanzibar ikiwa  ‘TUNZA MAZINGIRA, DUMISHA UASILI WAKE, KUFIKIA UCHUMI WA BULUU’