NA NASRA MANZI, WHVUM

KATIBU MKuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab amewataka wafanyakazi wa Shirika la Magazeti ya Serikali kujiongeza kitaaluma ili kuongeza ufanisi katika kazi zao.

Kauli hiyo ameitoa wakati alipofanya ziara ya utambulisho wa Mkurugenzi Utumishi wa Wizara hiyo pamoja na kujua changamoto na maendeleo ya Shirika hilo huko Maisara.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuendeleza ufanisi wa kazi pamoja na kumsaidia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika ujenzi wa Zanzibar.

Aidha alisema ni vyema wafanyakazi kuwa na nidhamu, uweledi, uwajibikaji pamoja na kutafuta mbinu za kitaaluma ambazo zitawaletea uimara katika utendaji wa kazi.

Pia alisema mashirikiano, umoja na upendo kwa wafanyakazi ni jambo muhimu kwani kutaleta mabadiliko ya kiutendaji, sambamba na kuachana na majungu ambayo hayana tija.

“Tufanyeni kazi kwa mashirikiano na tuacheni majungu yasioleta tija lengo kuiletea mafanikio wizara pamoja na serikali yetu”, alisema.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Khamis Abdalla Said alisema wizara itaendelea kuhakikisha haki za wafanyakazi zinapatikana kwa wakati.

Nae Mkuurugenzi Utumishi Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Nasriya Mohamed amewashauri wafanyakazi hao kuwa wazalendo wa nchi yao ili kuisaidia serikali kwa ajili ya kutengeneza bora.

Kwa upande wa wafanyakazi wa Shirika hilo waliiomba serikali kupitia Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo kuwatatulia changamoto zinazowakabili kwa ajili ya kupata haki zao kwa lengo la kuliletea mafanikio Shirika hilo.